47-Malaika: Kazi Za Malaika: (10)- Malaika Wenye Kuizuru Al-Baytul Ma’amuwr
Malaika
47: Kazi Za Malaika
(10)- Malaika Wenye Kuizuru Al-Baytul Ma’amuwr
Nyumba hii Allaah Ameiapia Aliposema:
"وَالْبَيْتِ الْمَعْمُورِ"
“Na Naapa kwa Nyumba yenye kuamiriwa nyakati zote (na Malaika)”. [At-Tuwr: 04]
Al-Baghawiy amesema: “Nyumba hii iko katika mbingu ya saba na imeitwa hivi kutokana na wingi wa Malaika wanaoikusudia. Iko mkabala na Al-Ka’abah kiwima, na utukuzo wake mbinguni ni sawa na utukuzo wa Al-Ka’abah hapa ardhini, na kila siku wanaingia humo Malaika elfu 70 kwa ajili ya kutufu na kuswali humo, kisha hawarudi tena humo milele”.
Imepokelewa toka kwa Maalik bin Swa-‘aswa-’ah kuhusiana na kisa cha Israa kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"رُفِعَ لِيَ الْبَيْتُ الْمَعْمُورُ فَقُلْتُ: يَا جِبْرِيلُ مَا هَذَا؟ قَالَ: هَذَا الْبَيْتُ الْمَعْمُورُ يَدْخُلُهُ كُلَّ يَوْمٍ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ إِذَا خَرَجُوا مِنْهُ لَمْ يَعُودُوا فِيهِ آخِرُ مَا عَلَيْهِمْ"
“Nilinyanyuliwa Al-Baytul Al-Ma-‘amuwr nikasema: Ee Jibriyl, nini hii? Akasema: Hii ni Al-Baytul Ma-‘amuwr, kila siku wanaingia ndani yake Malaika elfu sabini, na wakitoka humo hawarudi tena hadi wa mwisho wao”.
Imepokelewa pia toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akizungumzia kisa cha Israa amesema:
"ففُتِح لنا فإذا أنا بإبراهيمَ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم مُسنِدًا ظَهْرَه إلى البيتِ المعمورِ، وإذا هو يدخُلُه كلَّ يومٍ سبعون ألْفَ مَلَكٍ لا يعودون إليه"
“Tukafunguliwa (mbingu), na hapo nikamkuta Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) akiwa ameegemeza mgongo wake kwenye Al-Baytul Ma’amuwr ambayo wanaingia humo kila siku Malaika elfu sabini na hawarudi tena humo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (14082), Ibn Abiy Shaybah katika Al-Muswannaf (17883) na Abu Ya’alaa (3373)]
Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkuta Nabiy Ibraahiym (‘alayhis salaam) katika hali hiyo kwa kuwa yeye ndiye aliyeijenga Al-Ka’abah ya hapa ardhini, na hayo ndiyo malipo yake, kwani malipo ni kwa mujibu wa matendo.
As-Sam-’aaniy amesema: Kauli maarufu ni kwamba hiyo ni Nyumba iliyoko mbinguni. Limesemwa hili na Ibn ‘Abbaas na Mufassiruna wote, pia limehadithiwa toka kwa ‘Aliyy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaah ‘anhu).
An-Nawawiy amesema: “Hii ni dalili kubwa ya kuonyesha idadi kubwa mno ya Malaika rehmah na amani ziwe juu yao”.