48-Malaika: Kazi Za Malaika: (11)- Malaika Mwenye Kutoa Roho

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

48:   Kazi Za Malaika

 

(11)- Malaika Mwenye Kutoa Roho

 

Katika baadhi ya aathaar, Malaika mtoa roho (Malakul Mawt) ametajwa kama ‘Izraaiyl, lakini jina hili halijathibitishwa, si katika Qur-aan wala katika Sunnah.

 

Ibn Kathiyr amesema:  “Ama Malakul Mawt, yeye jina lake halijatajwa katika Qur-aan wala katika Hadiyth zilizo swahiyh, lakini ametajwa katika baadhi ya aathaar kama ni ‘Izraaiyl, na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Sheikh Bin Baaz (Allaah Amrehemu) aliulizwa kama katika Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) limethibiti jina la ‘Izraaiyl kama ni Malaika mtoa roho?  Naye alijibu akisema:  Sijui chochote kilichothibiti kuhusiana na hili, lakini lililotangaa baina ya Wanazuoni ni kuwa jina lake ni ‘Izraaiyl, lakini mimi sijui Hadiyth yoyote iliyo sahihi kwamba jina lake ni hilo, bali limetajwa kwenye aathaar dhaifu ambazo hazifai kuwa ni hoja”.

 

Ama Al-Albaaniy, yeye kasema:  “Malakul Mawt ndio jina lake lililotajwa ndani ya Qur-aan Tukufu.  Ama kumuita ‘Izraaiyl kama ilivyotangaa kwa watu, hilo halina asili, bali limechukuliwa toka kwenye Israaiyliyyaat (Hadiyth na riwaayah za kutunga toka kwenye Taurati na Injili”.

 

‘Abdulrahmaan Al-Barraak amesema:  “Jina hili la ‘Izraaiyl ni mashuhuri lakini halikuthibiti, bali majina ya Malaika yaliyothibiti ni Jibriyl, Miykaaiyl, Israafiyl, Maalik mlinzi wa moto, pia Munkar na Nakiyr, nao ni Malaika wawili wanaomuuliza maswali maiti kaburini”.

 

Malakul Mawt ametajwa katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ

 

Sema:  Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa”.  [As-Sajdah: 11].

 

Malaika huyu ana wasaidizi wake.  Hebu fikiria, katika kipindi cha saa 24 au dakika kadhaa, ni watu wangapi wanakufa duniani kote?  Hivyo ni lazima awe na wasaidizi wake.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

 

"حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ    •  ثُمَّ رُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۚ أَلَا لَهُ الْحُكْمُ وَهُوَ أَسْرَعُ الْحَاسِبِينَ"

 

Hata yanapomfikia mmoja wenu mauti, Wajumbe Wetu (Malaika) humfisha, nao hawafanyi taksiri   Kisha watarudishwa (wote waliofishwa) kwa Allaah Rabb wao wa haki.  Tanabahi!  Hukumu ni Yake Pekee; Naye ni Ni Mwepesi zaidi kuliko wote wanaohisabu.  [Al-An’aam: 61-62]

 

Malaika hawa hupokea amri toka kwa Malakul mawt ya kutoa roho ya mtu ambaye muda wake umefika, na utoaji huo unanasibishwa kwa Malakul Mawt kana kwamba yeye ndiye aliyetekeleza zoezi hilo moja kwa moja.  Ni kama vile mkuu wa jeshi anapoamuru askari wake kufanya operesheni fulani, yeye hashiriki, lakini zoezi hilo linanasibishwa kwake.

 

Na katika Az-Zumar, Allaah Amelinasibisha zoezi hili Kwake Yeye Mwenyewe Aliposema:

 

"اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا"

 

“Allaah Huzichukua roho wakati wa kufa kwake”.  [Az-Zumar: 42]

 

Na hapa hakuna ukinzani kati ya Aayaah, kwa kuwa hakuna yeyote anayekufa isipokuwa kwa kupenda Kwake Allaah.  Malaika hao wasingeweza kufanya kazi hiyo bila Yeye ‘Azza wa Jalla kutaka, na Yeye Ndiye pia Aliyeupanga muda wa kuishi wa kila kiumbe, hivyo basi mambo yote yananasibishwa Kwake.

 

Nafsi au roho kabla haijatoka, mtu hujiwa na Malaika wa rahmah wenye sanda na mafuta mazuri ya Peponi kama ni mwema.  Baada tu ya Malakul Mawt kuitoa roho yake, Malaika hao huichukua hapo kwa papo, wakaikafini na kisha wakaondoka nayo kwenda nayo juu.  Roho yake itakafiniwa na Malaika hao, na mwili wake utaoshwa, utakafiniwa, utaswaliwa na utazikwa na nduguze Waislamu.

 

Ama kafiri, roho yake itavikwa vile vile sanda ya motoni na kuwa na harufu mbaya ya kuchukiza mno.  Roho ikitoka tu, itadakwa na Malaika wa adhabu, na hapo safari ya mateso inaanzaHadiyth hii ya Al-Baraa bin ‘Aazib inathibitisha haya.  Amesema:

 

"خرَجْنا مع النَّبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم في جِنازةِ رَجُلٍ من الأنصارِ، فانتَهَينا إلى القبرِ ولَمَّا يُلحَدْ، فجلس رسولُ الله صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، وجلَسْنا حولَه كأنَّ على رُؤوسِنا الطيرَ، وفي يَدِه عودٌ يَنكُتُ في الأرضِ، فرفع رأسَه، فقالاستعيذوا باللهِ من عذابِ القَبرِ، مَرَّتينِ أو ثلاثًا، ثمَّ قال: إنَّ العبْدَ المؤمِنَ إذا كانَ في انْقِطاعٍ مِنَ الدُّنْيا، وإقْبالٍ مِنَ الآخِرَةِ، نزَلَ إليه مَلائكةٌ مِنَ السَّماءِ بِيضُ الوُجوهِ، كَأنَّ وُجوهَهُمُ الشَّمْسُ، معَهُم كَفَنٌ مِن أَكْفانِ الجَنَّةِ، وحَنُوطٌ  مِن حَنُوطِ الجَنَّةِ، حتَّى يَجْلِسوا مِنه مَدَّ البَصَرِ، ثمَّ يَجيءُ مَلَكُ المَوْتِ علَيه السَّلامُ، حتَّى يَجْلِسَ عندَ رَأْسِه، فيَقُولُ: أَيَّتُها النَّفْسُ الطَّيِّبَةُ، اخْرُجي إِلى مَغْفرةٍ مِنَ اللهِ ورِضْوانٍ. فتَخْرُجُ تَسِيلُ كَما تَسِيلُ القَطْرةُ مِن فِي السِّقَاءِ، فيَأْخُذُها، فإذا أخَذَها لم يَدَعُوها في يَدِه طَرْفةَ عينٍ حتَّى يَأخُذوها، فيَجْعَلوها في ذَلِك الكَفَنِ، وفي ذَلِك الحَنُوطِ، ويَخْرُجُ مِنها كَأَطْيبِ نَفْحةِ مِسْكٍ وُجِدَت على وَجْهِ الْأَرْضِ. فيَصْعَدونَ بِها"

 

“Tulitoka kwenda kumzika mwanaume wa Kianswaar pamoja na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Tulipofika kaburini, mwanandani ulikuwa bado unachimbwa.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakaa, nasi tukakaa pembezoni mwake kimya kana kwamba kuna ndege juu ya vichwa vyetu.  Rasuli alikuwa na kijiti mkononi mwake na akawa anakigonga gonja chini (kama vile mtu mwenye ghamu), kisha akanyanyua kichwa chake akasema:  Jilindeni kwa Allaah na adhabu ya kaburi, alisema mara mbili au tatu halafu akaendelea kusema:  Mja muumini akiwa katika hali ya kuondoka duniani na kuelekea aakhirah, Malaika wenye nyuso nyeupe mithili ya jua humteremkia toka mbinguni wakiwa na sanda kati ya sanda za Peponi pamoja na mafuta katika mafuta mazuri ya Peponi, na hukaa upeo wa macho toka pale alipo.  Kisha Malakul Mawt (‘Alayhis Salaam) huja na kukaa mbele ya kichwa chake na kumwambia:  Ee nafsi njema, toka uende kwenye maghfira ya Allaah na radhi Zake.  Roho hiyo itatoka ikichuruzika kama tone la maji linavyochuruzika toka chomboni, na Malakul Mawt huichukua, na anapoichukua haibaki kwenye mkono wake muda wa pepeso la jicho ila huchukuliwa na Malaika (wa rahmah) ambao wanaiweka kwenye sanda hiyo na kwenye mafuta hayo.  Kisha roho hiyo hutoka kwake harufu mzuri mno kama mnuso wa mafuta ya miski ambayo hakuna mfano wake juu ya uso wa ardhi, halafu hupanda nayo juu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Swahiyhul Jaami’i (1676)]

 

 

Share