49-Malaika: Kazi Za Malaika: (12)- Malaika Wanaowasaili Maiti Kaburini

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

49:   Kazi Za Malaika

 

(12)- Malaika Wanaowasaili Maiti Kaburini

 

Malaika hawa ni wawili na wanajulikana kama Munkar na Nakiyr.  Ni weusi wenye macho kibuluu, na humjia maiti ili kumuuliza baadhi ya maswali baada ya kuzikwa.  Ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamuru tumwombee maghfira ndugu yetu tuliyemzika ili asaa dua zetu zikamsaidia katika kukabiliana na mtihani huo mgumu na mazingira hayo ya kutisha anayokabiliana nayo kwa mara ya kwanza kabisa.  Huo ni miongoni mwa mitihani ya mwanzo inayotukabili ya aakhirah baada ya kupitia mitihani mingine ya hapa duniani.  Maswali wanayomuuliza maiti si magumu, ni ya kawaida tu, lakini yanaweza kuwa magumu kwa Muislamu mwenye kumwasi Allaah, na kama ni kafiri au mushrik, basi hatoweza kujibu lolote.  Amali njema za mja na kumcha Allaah ndiyo silaha zitakazomwezesha kuyajibu maswali hayo, na Allaah Ndiye Atakayempa uthabiti kama Anavyotuambia:

 

"يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ"

 

“Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah.  Na Allaah Huwaacha kupotoka madhalimu.  Na Allaah Anafanya Atakavyo”[Ibraahiym: 27]

 

 

Katika Hadiyth iliyopokelewa na Anas bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu), Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إنَّ العَبْدَ إذَا وُضِعَ في قَبْرِهِ وتَوَلَّى عنْه أصْحَابُهُ، وإنَّه لَيَسْمَعُ قَرْعَ نِعَالِهِمْ، أتَاهُ مَلَكَانِ فيُقْعِدَانِهِ، فَيَقُولَانِ: ما كُنْتَ تَقُولُ في هذا الرَّجُلِ؛ لِمُحَمَّدٍ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فأمَّا المُؤْمِنُ، فيَقولُ: أشْهَدُ أنَّه عبدُ اللَّهِ ورَسولُهُ، فيُقَالُ له: انْظُرْ إلى مَقْعَدِكَ مِنَ النَّارِ قدْ أبْدَلَكَ اللَّهُ به مَقْعَدًا مِنَ الجَنَّةِ، فَيَرَاهُما جَمِيعًا، وَأمَّا المُنَافِقُ والكَافِرُ فيُقَالُ له: ما كُنْتَ تَقُولُ في هذا الرَّجُلِ؟ فيَقولُ: لا أدْرِي، كُنْتُ أقُولُ ما يقولُ النَّاسُ، فيُقَالُ: لا دَرَيْتَ ولَا تَلَيْتَ، ويُضْرَبُ بمَطَارِقَ مِن حَدِيدٍ ضَرْبَةً، فَيَصِيحُ صَيْحَةً يَسْمَعُهَا مَن يَلِيهِ غيرَ الثَّقَلَيْنِ"  

 

“Mja anapowekwa katika kaburi lake na watu wake wakaondoka, na kwa hakika husikia mchakato wa viatu vyao, humjia Malaika wawili wakamkalisha, kisha humuuliza:  Ulikuwa unasema nini kuhusu mtu huyu?  Yaani Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Akiwa maiti ni Muumini atasema:  Ninashuhudia kwamba yeye ni Mja wa Allaah na Mtume Wake. Na hapo ataambiwa:  Angalia kwenye makazi yako motoni, Allaah Amekubadilishia kwayo kuwa makazi ya Peponi, naye atayaona makazi yote mawili.  Ama mnafiki na kafiri, yeye pia ataulizwa:  Ulikuwa unasema nini kuhusu mtu huyu?  Atasema:  Sijui, nilikuwa nasema yale wayasemayo watu.  Ataambiwa:  Hukujua wala hukusoma.  Kisha atapigwa nyundo ya chuma pigo moja kali (kati ya masikio yake mawili), na atapiga ukelele watakaousikia viumbe wote walio karibu yake isipokuwa majini na wanadamu”.  [Swahiyhul Jaami’i (1675)]

 

Hadiyth hii imegusia swali moja tu kumhusu Mtume (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini Hadiyth nyingine zinasema ataulizwa:  Nani Mola wako?  Ipi dini yako?  Nani Nabiy wako? 

 

Namwomba Allaah ‘Azza wa Jalla Atupe uthabiti tuweze kuyajibu maswali haya sawasawa, na tupite salama kwenye mtihani huo mgumu.

 

 

Share