51-Malaika: Kazi Za Malaika: (14)- Malaika Walinzi Na Malaika Wa Adhabu Wa Moto (Zabaaniyah)
Malaika
51: Kazi Za Malaika
(14)- Malaika Walinzi Na Malaika Wa Adhabu Wa Moto (Zabaaniyah)
Malaika mlinzi mkuu wa moto wa Jahannam ni Maalik. Allaah Ta’aalaa Anasema:
"وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ ۖ قَالَ إِنَّكُم مَّاكِثُونَ"
“Na wataita: Ee Maalik! (Mlinzi wa moto) Na Atumalize tufe Rabb wako. Atasema: Hakika nyinyi ni wenye kubakia kuishi humo”. [Az-Zukhruf: 77]
Huyu ana wasaidizi wake wanaojulikana kama Zabaaniyah. Hawa ni Malaika wa adhabu kwa watu wa motoni. Wana nguvu za kupindukia, wana maumbo na sauti za kutisha na kukera mno, na ni wakali mno. Allaah ‘Azza wa Jalla Amewataja katika Suwrat Al-‘Alaq Aliposema:
"سَنَدْعُ الزَّبَانِيَةَ"
“Nasi Tutawaita Az-Zabaaniyah (Malaika wa adhabu)”.
Malaika hawa watawapokea watu watakaoingia motoni. Sijui yatakuwa mapokezi ya aina gani ya kupokewa na Malaika kama hao! Bila shaka ni adhabu juu ya adhabu. Hapa duniani tunaona namna askari wanavyowapokea baadhi ya watu wanaoshukiwa tu kwa kosa vituoni au mahabusu kwa mateke na vipigo. Hali itakuwaje kwa hao watakaoswagwa kupelekwa motoni na Malaika hao! Allaah ‘Azza wa Jalla Anatuambia:
"وَسِيقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا فُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ رُسُلٌ مِّنكُمْ يَتْلُونَ عَلَيْكُمْ آيَاتِ رَبِّكُمْ وَيُنذِرُونَكُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَلَـٰكِنْ حَقَّتْ كَلِمَةُ الْعَذَابِ عَلَى الْكَافِرِينَ"
“Na wataswagwa wale waliokufuru kuelekea Jahannam makundi-makundi, mpaka watakapoifikia, itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Je, hawajakufikieni Rusuli miongoni mwenu, wakikusomeeni Aayaat za Rabb wenu, na wakikuonyeni kukutana na Siku yenu hii? Watasema: Ndio! Lakini neno la adhabu limethibiti juu ya makafiri”. [Az-Zumar: 71]
Juu ya moto wa Jahannam watakuwepo Malaika 19. Na hawa ni mbali na hao wengineo. Allaah Anatuambia:
"عَلَيْهَا تِسْعَةَ عَشَرَ"
“Juu yake wako (walinzi) kumi na tisa”. [Al-Muddath-thir: 30]
Namwomba Allaah ‘Azza wa Jalla Atuepushe tusije kuonana na viumbe hawa.