52-Malaika: Kazi Za Malaika: (15)- Malaika Wenye Kuwasaidia Manabii Na Mitume Na Kuwaangamiza Makafiri

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

                                                 52:   Kazi Za Malaika

 

(15)- Malaika Wenye Kuwasaidia Manabii Na Mitume Na Kuwaangamiza Makafiri

 

Dalili toka kwenye Qur-aan na Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinaonyeha kwamba Jibriyl (‘alayhis Salaam) alikuwa na jukumu la kuwasaidia, kuwatia nguvu na kuwanusuru Manabii na Mitume (‘alayhimus Salaam), lakini pia kupigana na maadui zao na kuwaangamiza.  Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَإِن تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ"

 

Na mkisaidiana dhidi yake, basi hakika Allaah Ndiye Mlinzi Msaidizi wake na Jibriyl na Waumini wema, na zaidi ya hayo, Malaika pia watasaidia”.  [At-Tahriym: 04]

 

Allaah, Jibriyl, Waumini wema pamoja na Malaika, wote wanamsaidia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Ikiwa hawa wote wako pamoja naye, basi ni nani ataweza kumdhuru?!  Na hii ni fadhila kubwa na sharafu adhimu kwa Bwana wa Mitume Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Aliyopewa na Mola wake.

 

Malaika huyu Jibriyl (‘Alayhis Salaam), Allaah Ta’aalaa Amemwelezea kama ni mwenye nguvu nyingi.  Amesema:

 

 

"عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ"

 

Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi”.  [An-Najm: 05]

 

Yaani, aliyemfundisha Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Qur-aan ni Jibriyl (‘alayhis Salaam) mwenye nguvu shadidi.

 

 

Inasimuliwa kwamba Malaika huyu Jibriyl, alin’goa miji au vijiji vya kaumu Lut, halafu akavipandisha hadi juu mbinguni, kisha akavipindua juu chini, vikaporomoka hadi chini ardhini.  Allaah Anasema:

 

 

"وَالْمُؤْتَفِكَةَ أَهْوَىٰ"

 

Na miji iliyopinduliwa, Ameiporomosha mbali mbali”.  [An-Najm: 53]

 

 

Ibn Jariyr akiizungumzia aayah hii anasema kwamba hiyo ni miji ya Sodom na Gomorrah ya kaumu Lut, Allaah Aliiporomosha, Akamwamrisha Jibriyl (‘alayhis salaam) ainyanyue toka ardhi ya saba kwa ubawa wake hadi juu mbinguni, kisha aiporomoshe toka huko ikiwa chini juu.

 

Lakini pia, aliwapigia ukelele mmoja tu watu wa Thamud wakabaki  majumbani mwao wameanguka kifudifudi (wamekufa).

 

Muhammad bin Ka’ab Al-Quradhiy amesema:  “Jibriyl (‘alayhis salaam) alitumwa kwenda kwenye miji iliyopinduliwa ya kaumu Lut.  Akaibeba kwa ubawa wake, halafu akapanda nayo juu kiasi cha hata wakazi wa mbinguni wakaweza kusikia sauti za mbwa wao wakibweka na sauti za kuku wao wakilia kwa hofu.  Kisha Allaah Akaiandamizia kwa mawe kama Anavyosema:

 

"فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ"

 

“Basi ilipokuja Amri Yetu, Tuliupindua (mji wao) juu chini, na Tukauteremshia mvua ya mawe ya udongo mgumu uliookwa yenye kuandamana”.   Allaah Akaiangamiza pamoja na walio pembezoni mwa miji hii ambayo ilikuwa ni mitano”

 

Na wakati Allaah Ta’aalaa Alipomwokoa Muwsaa (‘alayhis salaam) pamoja na watu wake aliokuwa nao, na Akamwangamiza adui yao Firauni pamoja na askari na wafuasi wake,  Jibriyl (‘alayhis salaam) alikuwepo hapo akisaidiaIbn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa amesema:  “Jibriyl alikuwa akishindilia tope la mchanga kwenye kinywa cha Firauni akihofia asije kutamka:  “Laa Ilaah Illa Allaah”.

 

Kadhalika, Jibriyl (‘alayhis salaam) alimtia nguvu Nabiy ‘Iysaa (‘alayhis salaam) kama Anavyosema Allaah:

 

"وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ"

 

“Na Tukamtia nguvu kwa Ruwhil-Qudus (Jibriyl (عليه السلام.  [Al-Baqarah: 87]

 

Vile vile, Rasuli (Swalla Allaah (‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwombea Hassaan bin Thaabit (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Allaah Ta’aalaa Amtie nguvu kupitia Jibriyl katika kumtetea yeye kwa mashairi dhidi ya matusi ya Maquraysh. 

 

Bibi ‘Aaishah amesema:

 

"كان ينافِحُ عن رَسولِ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم" 

 

“Alikuwa akimtetea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (kwa mashairi yake)[Muslim: (2490)] 

Isitoshe, Allaah Ta’aalaa Alimtia nguvu Nabiy Wake Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa pamoja na Waumini kupitia Jibriyl (‘alayhis salaam) katika baadhi ya vita.

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema Siku ya Badr:
.

"هذا جِبريلُ آخِذٌ برأسِ فَرَسِه، عليه أداةُ الحَربِ"  

 

“Huyu ni Jibriyl, amekamata kichwa cha farasi wake, amevalia zana za kivita”.   [Swahiyh Al-Bukhaariy: (3995)]

 

Hapa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwazindusha Maswahaba wake uwepo wa Jibriyl katika uwanja wa vita ili kuwapa ukakamavu na uimara zaidi, lakini pia kuwatuliza nyoyo. 

 

Kadhalika, katika Vita vya Makundi, Siku ya Khandaq, Jibriyl pia aliwasaidia Waumini.  Bibi ‘Aaishah amesema:

"فَلَمَّا رَجَعَ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم مِنَ الخَنْدَقِ وَضَعَ السِّلَاحَ، فَاغْتَسَلَ، فأتَاهُ جِبْرِيلُ وَهو يَنْفُضُ رَأْسَهُ مِنَ الغُبَارِ، فَقالَ: وَضَعْتَ السِّلَاحَ؟ وَاللَّهِ ما وَضَعْنَاهُ، اخْرُجْ إليهِم، فَقالَ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: فأيْنَ؟ فأشَارَ إلى بَنِي قُرَيْظَةَ، فَقَاتَلَهُمْ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فَنَزَلُوا علَى حُكْمِ رَسولِ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فَرَدَّ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم الحُكْمَ فيهم إلى سَعْدٍ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliporejea toka Vita vya Khandaq, aliirejesha silaha yake mahala pake, kisha akaoga.  Jibriyl akamjia huku akikun’guta vumbi kichwa chake.  Akamuuliza:  Umeweka silaha chini?  Naapa kwa Allaah, sisi bado hatujaweka silaha chini, toka uwafuate.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:  Wapi? Akamwashiria kwenda kwa Baniy Quraydhwah.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapambana nao mpaka wakasalimu amri kuwa chini ya utawala wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaurejeshea utawala kwa Sa’ad awaongoze”.   [Al-Bukhaariy (4122) na Muslim (1769)]

 

Isitoshe, Malaika wa milima pia alikuja kumsaidia Rasuli kama angetaka baada ya kupopolewa mawe na watu wa Taif alipokwenda kuwalingania dini na kuomba hifadhi yao.

 

Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alimuuliza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: 

 

"هَلْ أَتَى عَلَيْكَ يَوْمٌ كَانَ أَشَدَّ مِنْ يَوْمِ أُحُدٍ؟ قَالَ: ‏ لَقَدْ لَقِيتُ مِنْ قَوْمِكِ مَا لَقِيتُ، وَكَانَ أَشَدُّ مَا لَقِيتُ مِنْهُمْ يَوْمَ الْعَقَبَةِ، إِذْ عَرَضْتُ نَفْسِي عَلَى ابْنِ عَبْدِ يَالِيلَ بْنِ عَبْدِ كُلاَلٍ، فَلَمْ يُجِبْنِي إِلَى مَا أَرَدْتُ، فَانْطَلَقْتُ وَأَنَا مَهْمُومٌ عَلَى وَجْهِي، فَلَمْ أَسْتَفِقْ إِلاَّ وَأَنَا بِقَرْنِ الثَّعَالِبِ، فَرَفَعْتُ رَأْسِي، فَإِذَا أَنَا بِسَحَابَةٍ قَدْ أَظَلَّتْنِي، فَنَظَرْتُ فَإِذَا فِيهَا جِبْرِيلُ فَنَادَانِي فَقَالَ إِنَّ اللَّهَ قَدْ سَمِعَ قَوْلَ قَوْمِكَ لَكَ وَمَا رَدُّوا عَلَيْكَ، وَقَدْ بَعَثَ إِلَيْكَ مَلَكَ الْجِبَالِ لِتَأْمُرَهُ بِمَا شِئْتَ فِيهِمْ، فَنَادَانِي مَلَكُ الْجِبَالِ، فَسَلَّمَ عَلَىَّ ثُمَّ قَالَ يَا مُحَمَّدُ، فَقَالَ ذَلِكَ فِيمَا شِئْتَ، إِنْ شِئْتَ أَنْ أُطْبِقَ عَلَيْهِمِ الأَخْشَبَيْنِ، فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم بَلْ أَرْجُو أَنْ يُخْرِجَ اللَّهُ مِنْ أَصْلاَبِهِمْ مَنْ يَعْبُدُ اللَّهَ وَحْدَهُ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا‏"‏‏.‏

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Je uliwahi kukutana na siku ngumu zaidi kuliko Siku ya Vita vya Uhud?  Rasuli akasema:  Hakika nimepata mateso mengi na adha nyingi sana toka kwa watu wako (Maquraysh).  Lakini siku ngumu zaidi niliyopambana nayo toka kwao ilikuwa siku ya ‘Aqabah.  Ni pale nilipojitambulisha kwa Ibn ‘Abdi Yaaliyla bin ‘Abdi Kulaal lakini hakunijibu matakwa yangu.  Nikaondoka na huzuni kubwa mno, na sikuzindukana ila baada ya kufika Qarn Ath-Tha’aalib.  Nikanyanyua kichwa changu na kushtukizwa kuona wingu limenifunika kwa kivuli chake.  Nikaliangalia na tahamaki nikamwona Jibriyl ndani yake.  Akaniita na kuniambia:  Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Amesikia waliyokwambia watu wako, na majibu waliyokupa,  na Yeye Amekutumia Malaika wa milima ili umwamuru lolote ulitakalo.  Malaika wa milima akaniita na kunisalimia, kisha akasema:  Ee Muhammad!  Hakika Allaah Amesikia maneno waliyokwambia watu wako, na mimi ndiye Malaika wa milima, na Mola wako Amenituma kwako ili uniamuru lolote utakalo kwa watu hao.  Ukitaka nitawafudikiza kwa milima miwili, basi nitawafudikiza.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  Bali ninatumai Allaah Atatoa toka kwenye migongo yao watakaomwabudu Allaah Peke Yake na hawatamshirikisha na chochote”.  [Swahiyhul Bukhaariy (3231)]

 

Mwisho, tunauliza:  Kuna hikma gani ya Malaika kupigana pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati tunajua kwamba Jibriyl ana uwezo wa kuwaangamiza makafiri wote kwa unyoya mmoja tu wa ubawa wake?!

 

Jibu nakuachia mpenzi msomaji ulitafute mwenyewe.

 

 

Share