53-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (01)- Malaika Wanawapenda Waumini

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

53:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini

 

(01)-  Malaika Wanawapenda Waumini

 

Allaah Ta’aalaa kama Alivyo na sifa ya kupenda, pia vile vile Amewapa Malaika Wake sifa ya kuwapenda Waumini.  Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu), Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ اللَّهَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى إِذَا أَحَبَّ عَبْدًا نَادَى جِبْرِيلَ: إِنَّ اللَّهَ قَدْ أَحَبَّ فُلاَنًا فَأَحِبَّهُ فَيُحِبُّهُ جِبْرِيلُ، ثُمَّ يُنَادِي جِبْرِيلُ فِي السَّمَاءِ: إِنَّ اللَّهَ قَدْ أَحَبَّ فُلاَنًا فَأَحِبُّوهُ، فَيُحِبُّهُ أَهْلُ السَّمَاءِ، وَيُوضَعُ لَهُ الْقَبُولُ فِي أَهْلِ الأَرْضِ"

 

“Allaah Anapompenda mja, Humnadia Jibriyl:  Hakika Allaah Anampenda fulani, basi na wewe mpende, na yeye Jibriyl humpenda mtu huyo.  Halafu naye Jibriyl huwanadia wakazi wa mbinguni (Malaika):  Hakika Allaah Anampenda fulani, basi na nyinyi mpendeni, na wakazi hao wa mbinguni humpenda.  Kisha huandikiwa maridhio kwa wakazi wa ardhi”.   [Swahiyh Muslim (2637)]

 

Maridhio yanayokusudiwa hapa ni mapenzi ya watu kwake, yaani nyoyo zao zitajazwa mapenzi ya kumpenda yeye.  Na watakaompenda ni Waumini, wachaMungu, si kila mmoja.

 

Bila shaka, kwa mfano, mwanamke akijua kwamba mume wake anampenda na anamtaja kwa jina kwa watu wake, ni furaha ilioje inayoingia ndani ya moyo wake!  Na wewe ndugu yangu mtukufu! Unapojua kwamba mkuu wa nchi, au waziri, au mheshimiwa yeyote, au bosi wako amekupenda na akakutaja mbele ya baraza lake, je, furaha yako inakuwaje?  Basi hali itakuwa vipi ikiwa Allaah Mola wa mbingu na ardhi Ndiye Aliyekupenda, na Akalitaja jina lako kwa Jibriyl, na kisha Jibriyl naye akawajuza Malaika wote wa mbinguni, na akawatajia jina lako, ukawa umejulikana kote huko, na akawataka nao wakupende, ni hadhi na furaha ilioje hiyo?!

 

Basi hongera kwa wale ambao Allaah ‘Azza wa Jalla Amewapenda, na Akawaamrisha Malaika Wake wampende, na akaandikiwa kupendwa na watu wa ardhi.  Na hawa ni wachaji na watenda mema wenye kupita juu ya njia Yake iliyonyooka.

 

 

Share