54-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (02)– Malaika Wanawatia Nguvu Waumini Na Kuwaelekeza
Malaika
54: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini
(02)– Malaika Wanawatia Nguvu Waumini Na Kuwaelekeza
Jibriyl (‘alayhis salaam) alimtia nguvu Nabiy ‘Iysaa (‘alayhis salaam) katika jukumu la kuwafikishia Baniy Israaiyl Dini ya Allaah. Allaah Anasema:
"وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ"
“Na Tukampa ‘Iysaa mwana wa Maryam hoja bayana na Tukamtia nguvu kwa Ruwhil-Qudus (Jibriyl (عليه السلام”. [Al-Baqarah: 87]
Mufassiruna wengi wamesema kwamba “Ruwhul Qudus” ni Jibriyl (‘alayhis salaam).
Toka kwa Hassaan bin Thaabit (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:
"يا حَسَّانُ، أجِبْ عن رسولِ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، اللهُمَّ أيِّدْه برُوحِ القُدُسِ"
“Ee Hassaan! Mtetee (kwa mashairi) Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) . Ee Allaah! Mtie nguvu kwa Ruwhul Qudus”. [Swahiyhul Bukhaariy (3212]
Ibn Hubayrah amesema: “Hadiyth hii ni dalili kwamba Allaah Anaweza kumtia nguvu mshairi kupitia kwa Jibriyl (‘alayhis salaam) kwa kumlinda na shetani asije kupenyeza maneno yasiyofaa kwenye ulimi wake.
Toka kwa Abu Hurayrah: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لأطوفَنَّ الليلةَ بمائةِ امرأةٍ، تَلِدُ كُلُّ امرأةٍ غُلامًا يقاتِلُ في سَبيلِ اللهِ. فقال له الملَكُ: قُلْ: إن شاء اللهُ، فلم يقُلْ، ونَسِيَ، فأطاف بهِنَّ، ولم تلِدْ إلَّا امرأةٌ منهنَّ نِصفَ إنسانٍ. قال النَّبيُّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: لو قال: إن شاء اللهُ، لم يحنَثْ، وكان أرجى لحاجَتِه"
“Kwamba Sulaymaan (‘alayhis salaam) alisema: (Naapa kwa Allaah) nitawazungukia (nitawaingilia) wanawake 100, na kila mwanamke atazaa kijana atakayepigana katika Njia ya Allaah. Malaika akamwambia: Sema In Shaa Allaah. Hakusema (kwa ulimi) na akasahau. Akawazungukia, na hakuna aliyezaa kati yao isipokuwa mmoja tu aliyezaa nusu mtu”. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Kama angelisema In Shaa Allaah, basi tarajio lake lisingepita tupu, na neno hilo lingempa matumaini zaidi ya haja yake”. [Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (3424) na Muslim (1654)]
Hapa tunaona namna Malaika alivyomkumbusha na kumwelekeza Nabiy Sulaymaan (‘alayhis salaam) atamke neno hilo. Neno hilo alilisemea moyoni akalitegemeza kwa Allaah, lakini hakulitamka ulimini, kwani haiwezekani Nabiy kama yeye kughafilika na jambo kama hilo. Na matokeo yake yakawa ndiyo hayo, hakuna aliyezaa isipokuwa huyo mmoja tu aliyezaa nusu mtu. Hiyo pia ni katika mitihani ya Allaah kwa Waja Wake na mafunzo kwao.