55-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (03)– Malaika Wanawaombea Dua Waumini
Malaika
55: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini
(03)– Malaika Wanawaombea Dua Waumini
Allaah Ta’aalaa Ametueleza kwamba Malaika Wake wanamswalia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale Aliposema:
"إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ"
”Hakika Allaah na Malaika Wake Wanamswalia Nabiy”. [Al-Ahzaab: 56]
Ametueleza tena kwamba Malaika hao wanawaswalia Waumini pia Aliposema:
"هُوَ الَّذِي يُصَلِّي عَلَيْكُمْ وَمَلَائِكَتُهُ لِيُخْرِجَكُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا"
“Yeye (Allaah) Ndiye Anakurehemuni, na Malaika Wake (wanakuombeeni maghfirah na rahmah) ili Akutoeni kutoka katika viza kuingia katika Nuru. Naye daima Ni Mwenye Kurehemu Waumini”. [Al-Ahzaab: 43]
Maana ya Allaah kuwaswalia Waja Wake ni kuwasifia na kuwataja vyema kwa Malaika Wake. Ama Malaika kuwaswalia waja, ni kuwaombea rahmah na maghfirah, na hili lina athari njema kwa Waumini ambapo kama inavyoeleza aayah hii, ni kwamba linapelekea Waumini kutolewa kwenye giza la ukafiri na kuingizwa kwenye nuru ya iymaan.
As-Sa’adiy amesema: “Kati ya Rehma Zake na Upole Wake kwa Waumini, Allaah Amejaalia Yeye kuwasifia kwa Malaika Wake, na Malaika hao kuwaombea maghfira na rahmah kuwa ni sababu ya kuwatoa toka kwenye giza za madhambi na ujinga kwenda kwenye nuru ya iymaan, elimu, utendaji mwema wa amali, na kuwezeshwa kwa yanayomridhisha Allaah. Hii ni moja kati ya neema kubwa kabisa ambazo Allaah Amewaneemesha kwazo Waja Wake watiifu ambazo zinawazindusha wazishukuru na wakithirishe kumdhukuru Allaah Aliyewatunuku.
Yafuatayo ni miongoni mwa mambo ambayo yatakuingiza ndani ya wigo wa kuombewa maghfirah na Malaika.
1- Kusubiri swala ya jamaa msikitini na kukaa baada ya kumalizika swala. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ الْمَلاَئِكَةَ تُصَلِّي عَلَى أَحَدِكُمْ مَا دَامَ فِي مُصَلاَّهُ الَّذِي صَلَّى فِيهِ مَا لَمْ يُحْدِثِ : اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ، اللَّهُمَّ ارْحَمْهُ"
“Hakika Malaika wanamwombea mmoja wenu madhali amebakia sehemu yake aliyoswalia na kuwa hajatengukwa na wudhuu wake. (Wanasema): Ee Allaah, Mghufurie, ee Allaah Mrehemu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (659) na Muslim (649)]
Mwanamke anaweza kuipata fadhila hii kama atakuwa na sehemu yake mahsusi ya kuswalia nyumbani kwake.
2- Kuswali safu ya kwanza.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الصَّفِّ الْأَوَّلِ"
“Hakika Allaah na Malaika Wake Huwaswalia wanaoswali safu ya kwanza”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Ibn Maajah]
Kuwaswalia hapa kuna maana ya kwamba, kwa upande wa Allaah ni kuwasifu na kuwarehemu, na kwa Malaika ni kuwaombea maghfirah.
3- Kutafuta ‘ilmu.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"مَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَطْلُبُ فِيهِ عِلْمًا سَلَكَ اللَّهُ بِهِ طَرِيقًا مِنْ طُرُقِ الْجَنَّةِ وَإِنَّ الْمَلاَئِكَةَ لَتَضَعُ أَجْنِحَتَهَا رِضًا لِطَالِبِ الْعِلْمِ وَإِنَّ الْعَالِمَ لَيَسْتَغْفِرُ لَهُ مَنْ فِي السَّمَوَاتِ وَمَنْ فِي الأَرْضِ وَالْحِيتَانُ فِي جَوْفِ الْمَاء"
“Mwenye kupita njia kwa lengo la kutafuta ‘ilmu, basi Allaah Atampitisha kwayo njia katika njia za Peponi. Na kwa hakika Malaika hushusha mbawa zao kuonyesha kufurahishwa kwao na mwanafunzi mtafutaji ‘ilmu. Na kwa hakika (pia), aliyeelimika, huombewa maghfirah na walioko mbinguni na walioko ardhini, na (hata) samaki walioko ndani ya kina cha maji”. [Sunan Abu Daawuwd].
Angalia hapa, si tu kwamba anapewa hishma kubwa na Malaika ya kushushiwa mbawa zao, bali hata viumbe vyote vilivyoko mbinguni kati ya Malaika wengineo wakiwemo wale wabebao ‘Arshi ya Allaah, pamoja na viumbe vinginevyo tusivyovijua huko, mbali na viumbe vyote vilivyoko ardhini hata vile tunavyovidharau kama nzi, panya, chawa na kadhalika, isitoshe na vyote vilivyoko ardhini, -vyote hivyo kwa wingi wote huo wa idadi isiyoweza kukokotoleka- vinamwombea maghfirah mwanafunzi anayetafuta ‘ilmu. Na ‘ilmu inayolengwa hapa ni ‘ilmu ya dini, kwani hiyo ndiyo itakayomwongoza Muislamu katika ‘aqiydah safi, atajua vyema mambo yote ya ‘ibaadah kuanzia twahara, swala, zakah, funga, hijja na mengineyo yote kuhusu kusoma Qur-aan kama inavyotakikana, Hadiyth za Rasuli na kadhalika. Haya ndiyo yatakayomfanya kuishi kwa amani hapa duniani na kesho aakhirah.
4- Kufundisha watu mambo ya kheri.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ اللَّهَ وَمَلاَئِكَتَهُ وَأَهْلَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ حَتَّى النَّمْلَةَ فِي جُحْرِهَا وَحَتَّى الْحُوتَ لَيُصَلُّونَ عَلَى مُعَلِّمِ النَّاسِ الْخَيْرَ"
“Hakika Allaah na Malaika Wake, pamoja na wakazi wa mbingu na ardhi, hata mdudu chungu katika shimo lake, na hata samaki, wanamwombea mwenye kuwafundisha watu mambo ya kheri”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2685) na At-Twabaraaniy (8/278)]
Mwalimu wa mambo ya kheri anayekusudiwa hapa ni Mwanachuoni, kwani yeye huwafundisha watu Maamrisho ya Allaah na kuwaonyesha Makatazo Yake ili wayaepuke, na mambo mengineyo yatakayowafaa katika dunia yao na aakhirah yao.
Ni wangapi kati yao wameshafariki zamani, lakini elimu zao hadi leo zinaendelea kuwanufaisha Waislamu. Na hii ina maana kuwa bado nao wanaendelea kuombewa na wote waliotajwa katika Hadiyth hii ingawa wako makaburini!
Lakini pia, hata yeyote anayesambaza elimu ya dini kwa njia ya mitandao kama tunavyoona vijana wetu hivi leo, basi wanaingia ndani ya duara la wigo huu, kuanzia wanaotarjumi, wanao-edit, wanaosambaza na kadhalika. Allaah Awalipe wote jazaa njema.
5- Kumswalia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُصَلِّي عَلَىَّ إِلاَّ صَلَّتْ عَلَيْهِ الْمَلاَئِكَةُ مَا صَلَّى عَلَىَّ فَلْيُقِلَّ الْعَبْدُ مِنْ ذَلِكَ أَوْ لِيُكْثِرْ"
“Hakuna Muislamu yeyote anayeniswalia isipokuwa Malaika nao humswalia madhali anaendelea kuniswalia. Basi na mja afanye uchache kwa hilo, au akithirishe”. [Hadiyth Hasan. Ibn Maajah]
6- Kumzuru mgonjwa
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"مَا مِنْ رَجُلٍ يَعُودُ مَرِيضًا مُمْسِيًا إِلاَّ خَرَجَ مَعَهُ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ يَسْتَغْفِرُونَ لَهُ حَتَّى يُصْبِحَ وَكَانَ لَهُ خَرِيفٌ فِي الْجَنَّةِ وَمَنْ أَتَاهُ مُصْبِحًا خَرَجَ مَعَهُ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ يَسْتَغْفِرُونَ لَهُ حَتَّى يُمْسِيَ وَكَانَ لَهُ خَرِيفٌ فِي الْجَنَّةِ"
“Hakuna mtu yeyote anayemzuru mgonjwa wakati wa jioni, isipokuwa hutoka pamoja naye Malaika elfu sabini wanaomwombea maghfira mpaka apambaukiwe asubuhi, na atapata pia bustani iliyosheheni matunda Peponi. Na atakayemwendea asubuhi, hutoka pamoja naye Malaika elfu sabini wanaomwombea maghfira mpaka jioni, na atapata bustani iliyosheheni matunda Peponi”. [Hadiyth Hasan. Swahiyh Abu Daawuwd]
7- Wanaokula daku
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إنَّ اللهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّوْنَ عَلَى المُتَسَحِّرِيْنَ"
“Hakika Allaah na Malaika Wake wanawaswalia wenye kula daku”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Hibaan (3467)]
Kuswaliwa na Allaah kuwasifu na kuwarehemu, na Malaika ni kuombewa maghfirah kwa Allaah.
Daku ni barakah. Si lazima kula mlo kamili wa shibe, bali inatosha hata kwa funda la maji ili kupata kusifiwa na Allaah na kuombewa maghfirah na Malaika Wake.