56-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (04)– Malaika Wanaitikia “Aamiyn” Kwa Dua Za Waumini

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

56:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini

 

(04)– Malaika Wanaitikia “Aamiyn” Kwa Dua Za Waumini

 

Malaika huitikia “aamiyn” kwa du’aa wanazoomba Waumini.  Na kwa kuitikia huku, du’aa inakuwa karibu zaidi kujibiwa kwa Idhni ya Allaah Ta’aalaa.

 

Katika Hadiyth iliyopokelewa na Abud Dardaai (Radhwiya Allaah ‘anhu), Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"دعوةُ الْمُسْلِمِ لِأَخِيهِ بِظَهْرِ الْغَيْبِ مُسْتَجَابَةٌ عِنْدَ رَأْسِهِ مَلَكٌ مُوَكَّلٌ كُلَّمَا دَعَا لِأَخِيهِ بِخَيْرٍ قَالَ الْمَلَكُ الْمُوَكَّلُ بِهِ: آمِينَ وَلَكَ بِمِثْلٍ" 

 

“Du’aa ya siri ya mtu Muislamu kwa nduguye ni yenye kujibiwa.  Huwepo Malaika mteuliwa kwenye kichwa chake, kila anapomwombea nduguye kheri, Malaika huyu mteuliwa kwa ajili yake husema:  “Aamiyn”, na wewe upate kama hilo”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imesimuliwa na Muslim]

 

Toka kwa Ummu Salamah:  “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا حَضَرْتُمُ الْمَرِيضَ أَو الْمَيِّت فَقولُوا خيرا فَإِن الْمَلَائِكَةَ يُؤَمِّنُونَ عَلَى مَا تَقُولُونَ"

 

“Mkiwepo kwa mgonjwa au maiti, basi waombeeni kheri, kwani Malaika huitikia “aamiyn” kwa mnaloliomba”.  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim (919)]

 

“Aamiyn maana yake ni: “Ee Allaah, Itikia”.

 

Abul ‘Abbaas Al-Qurtubiy kasema:  “Ulamaa wetu wanapendelea watu watakaokuwepo karibu na mtu wakati anapokaribia kufariki, wawe ni watu wema na watu wa kheri ili wapate kumkumbusha, na wamwombee yeye pamoja na ndugu na jamaa zake wahusika yaliyo ya kheri, kwani hapo itakutana du’aa yao na itikio la “aamiyn” la Malaika, na hivyo basi maiti pamoja na ndugu na jamaa zake hufaidika”.

 

 

Share