57-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (05)– Malaika Wanawaombea Maghfirah Waumini

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

57:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini  

 

(05)– Malaika Wanawaombea Maghfirah Waumini

 

Allaah Ta’aalaa Anatueleza katika Qur-aan Tukufu kwamba Malaika Wake wanawaombea maghfirah walioko ardhini Akituambia:

 

"تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِن فَوْقِهِنَّ ۚ وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ"

 

Zinakaribia mbingu kuraruka moja juu ya nyingine, na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini. Tanabahi! Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu”[Ash-Shuwraa: 05]

 

Wanaoombewa bila shaka ni Waumini walioko kwenye njia iliyonyooka ambayo inamridhisha Allaah, na si watu wote.  Hii ni katika Fadhla kubwa za Allaah kwetu ikiwa tutashikamana na Maamrisho Yake na kujiepusha na Makatazo Yake.  Inakuwa ni zawadi kwetu kwa kuwajibika huko.

 

Malaika wenye kufanya hivyo ni wale wenye kubeba ‘Arshi ya Allaah Ta’aalaa kama Anavyotuambia:

 

"الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ"

 

(Malaika) ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih na kumhimidi Rabbi wao, na wanamwamini, na wanawaombea maghfirah wale walioamini (wakisema):  Rabb wetu!  Umekienea kila kitu kwa rahmah na ujuzi, basi Waghufurie wale waliotubu, na wakafuata njia Yako, na Wakinge na adhabu ya moto uwakao vikali mno”.  [Ghaafir: 07]

 

Baadhi ya Mufassiruna wamesema kwamba si wanaobeba ‘Arshi tu, bali ni Malaika wote.

 

Al-Qurtubiy amesema:  “Yahyaa bin Mu’aadh Ar-Raaziy aliwaambia wenzake kuhusiana na aayah hii:  Ifahamuni vyema, kwani hakuna kinga duniani kote yenye kutumainiwa zaidi kuliko aayah hii.  Hakika Malaika mmoja tu, lau atamwomba Allaah Awaghufurie Waumini wote, basi Atawaghufiria.  Basi hali ikoje ikiwa Malaika wote pamoja na wabebao ‘Arshi wanawaombea maghfirah Waumini?!”

 

Naye Khalaf bin Hishaam Al-Bazzaaz Al-Qaariy amesema:  “Nilikuwa namsomea Saliym bin ‘Iysaa.  Nilipofika:

 

وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا

 

“Na wanawaombea maghfirah wale walioamini” alilia, kisha akasema: Ee Khalaf!  Ni utukuzo ulioje wa Muislamu kwa Allaah!  Yuko amelala kitandani mwake na huku Malaika Wake wanamwombea maghfirah!”

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"إِنَّ الْمَلاَئِكَةَ تُصَلِّي عَلَى أَحَدِكُمْ مَا دَامَ فِي مُصَلاَّهُ الَّذِي صَلَّى فِيهِ مَا لَمْ يُحْدِثِ : اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ، اللَّهُمَّ ارْحَمْهُ"

 

“Hakika Malaika wanamwombea mmoja wenu madhali amebakia sehemu yake aliyoswalia na kuwa hajatengukwa na wudhuu wake. (Wanasema):  Ee Allaah Mghufurie, ee Allaah Mrehemu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (659) na Muslim (649)]

 

 

Share