58-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (06)– Malaika Wanahudhuria Vikao Vya Ki’ilmu, Halaqah Za Dhikri, Na Huwafunika Wahusika Kwa Mbawa Zao

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

58:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini  

 

(06)– Malaika Wanahudhuria Vikao Vya Ki’ilmu, Halaqah Za Dhikri, Na Huwafunika Wahusika Kwa Mbawa Zao

 

Abu Hurayrah amesema:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ لِلَّهِ مَلاَئِكَةً يَطُوفُونَ فِي الطُّرُقِ، يَلْتَمِسُونَ أَهْلَ الذِّكْرِ، فَإِذَا وَجَدُوا قَوْمًا يَذْكُرُونَ اللَّهَ تَنَادَوْا هَلُمُّوا إِلَى حَاجَتِكُمْ‏.‏ قَالَ: فَيَحُفُّونَهُمْ بِأَجْنِحَتِهِمْ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا"

 

“Hakika Allaah Ana Malaika wanaozunguka majiani kuwatafuta watu wa dhikri.  Wanapowapata watu wanaomdhukuru Allaah huitana wakisema:  Haya njooni kwenye lile mlitafutalo.  Na hapo huwazungushia mbawa zao hadi kwenye mbingu ya dunia”.  [Swahiyhul Bukhaariy (6408)] 

 

Abu Hurayrah amesema tena:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"مَا اجْتَمَعَ قَوْمٌ فِي بَيْتٍ مِنْ بُيُوتِ اللَّهِ تَعَالَى يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّهِ وَيَتَدَارَسُونَهُ بَيْنَهُمْ إِلاَّ نَزَلَتْ عَلَيْهِمُ السَّكِينَةُ وَغَشِيَتْهُمُ الرَّحْمَةُ وَحَفَّتْهُمُ الْمَلاَئِكَةُ وَذَكَرَهُمُ اللَّهُ فِيمَنْ عِنْدَهُ ‏"‏‏.‏

 

“Hawakusanyiki watu katika Nyumba yoyote katika Nyumba za Allaah ili kusoma na kufundishana Kitabu cha Allaah, isipokuwa huwateremkia utulivu,  rahmah huwafunika, Malaika huwazunguka, na Allaah Huwataja kwa wale walio Kwake (Malaika)”.  [Muslim (2699)]

 

Amali njema ndio sababu ya Malaika kuwa karibu na Waumini.  Na lau kama Waumini wangeendelea kuwa katika hali ya juu kabisa ya utakasifu wa kiroho, basi wangelifikia ngazi ya kuweza kuwaona Malaika, kusalimiana nao na kupeana nao mikono.  Imepokelewa toka kwa Handhwalah Al-Usaydiy kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"الَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ تَدُومُونَ عَلَى مَا تَكُونُونَ عِنْدِي وَفِي الذِّكْرِ لَصَافَحَتْكُمُ الْمَلَائِكَةُ عَلَى فُرُشِكُمْ وَفِي طُرُقِكُمْ وَلَكِنْ يَا حَنْظَلَةُ سَاعَةٌ وَسَاعَةٌ"

 

“Naapa kwa Yule Ambaye Nafsi yangu iko Mkononi Mwake, lau mtadumu na hali mnayokuwa nayo wakati mnapokuwa kwangu na katika kumdhukuru Allaah, basi Malaika wangeliwapeni mikono mkiwa vitandani mwenu na majiani mwenu.  Lakini, ee Handhwalah, kuna saa (ya kusabilia moyo wako wote kwa Allaah) na kuna saa (ya kushughulikia mambo ya dunia yako)”.  [Muslim: 43] 

 

 

Share