59-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (07)– Malaika Wanasajili Majina Ya Wenye Kuhudhuria Swalah Ya Ijumaa
Malaika
59: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini
(07)– Malaika Wanasajili Majina Ya Wenye Kuhudhuria Swalah Ya Ijumaa
Malaika wanahudhuria Misikitini Siku ya Ijumaa na kusimama kwenye milango yake ili kuwasajili wanaoingia mmoja baada ya mwingine.
Abu Hurayrah: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا كَانَ يَوْمُ الْجُمُعَةِ وَقَفَتِ الْمَلَائِكَةُ عَلَى بَابِ الْمَسْجِدِ يَكْتُبُونَ الْأَوَّلَ فَالْأَوَّلَ"
“Inapokuwa Siku ya Ijumaa, Malaika husimama kwenye milango ya Msikiti na kuwasajili (wanaoingia) mmoja baada ya mwingine”. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Toka kwa Abu Hurayrah: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
إِذَا كَانَ يَوْمُ الْجُمُعَةِ، وَقَفَتِ الْمَلاَئِكَةُ عَلَى باب الْمَسْجِدِ يَكْتُبُونَ الأَوَّلَ فَالأَوَّلَ، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ طَوَوْا صُحُفَهُمْ، وَيَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ"
“Inapokuwa Siku ya Ijumaa, Malaika husimama kwenye mlango wa Msikiti na kusajili (wanaoingia) mmoja baada ya mwingine. Na khatibu anapochomoza, huyakunja madaftari yao na kusikiliza khutba (na yaliyomo humo katika utajo wa Allaah)”. [Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)]
Rasuli (Swalla Allaah ‘;alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمْعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ، ثُمَّ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الأُوْلَى فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الرَّابِعَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ دَجَاجَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الْخَامِسَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَيْضَةً، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ حَضَرَتِ الْمَلاَئِكَةُ يَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ "
“Mwenye kuoga kikamilifu siku ya Ijumaa kama anavyofanya katika ghuslu ya janaba, kisha akaenda (Msikitini) katika saa la mwanzo, basi anakuwa kama ametoa swadaqah ngamia, na mwenye kwenda saa la pili, anakuwa kama ametoa swadaqah ng’ombe, na mwenye kwenda saa la tatu, anakuwa kama ametoa swadaqah kondoo dume mwenye pembe, na mwenye kwenda saa la nne, anakuwa kama ametoa swadaqah kuku, na mwenye kwenda saa la tano, anakuwa kama ametoa swadaqah yai. Na Imamu anapotokeza (akapanda mimbari), Malaika huingia na kuketi kusikiliza utajo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)]
An-Nawawiy amesema: “Malaika hawa si wale wenye kumlinda mtu, bali hawa ni maalum kwa kusajili wanaohudhuria Swalaatul Jum’ah”.