61-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (09)– Malaika Wanapokezana Zamu Usiku Na Mchana Kuwafuatilia Waumini

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

61:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini  

 

(09)– Malaika Wanapokezana Zamu Usiku Na Mchana Kuwafuatilia Waumini

 

Kuna Malaika wanaozunguka kwenye njia na barabara kutafuta vikao vya dhikri.  Kuna wengineo wanaohudhuria Swalah za Ijumaa na Swalah za jamaa kwa zamu; kundi moja linakuja na jingine linaondoka.  Kadhalika, Malaika hawa hukusanyika pamoja katika Swalah ya Alfajiri na Swalah ya Alasiri.

 

Toka kwa Abu Hurayrah:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"يَتَعَاقَبُونَ فِيكُمْ مَلاَئِكَةٌ بِاللَّيْلِ وَمَلاَئِكَةٌ بِالنَّهَارِ وَيَجْتَمِعُونَ فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ وَصَلاَةِ الْعَصْرِ ثُمَّ يَعْرُجُ الَّذِينَ بَاتُوا فِيكُمْ فَيَسْأَلُهُمْ رَبُّهُمْ وَهُوَ أَعْلَمُ بِهِمْ كَيْفَ تَرَكْتُمْ عِبَادِي فَيَقُولُونَ تَرَكْنَاهُمْ وَهُمْ يُصَلُّونَ وَأَتَيْنَاهُمْ وَهُمْ يُصَلُّونَ"

 

Wanaandamana kwa zamu kwenu Malaika usiku na Malaika mchana, na wote hao wanajumuika katika Swalah ya Alfajiri na Swalah ya Alasiri, kisha wale waliokesha kwenu hupanda na Mola wao Huwauliza ilhali Yeye Anajua zaidi hali yao:  Vipi mmewaacha Waja Wangu?  Malaika hujibu:  Tumewaacha wakiwa wanaswali, na tumewajia wakiwa wanaswali”.  [Al-Bukhaariy (7486) na Muslim (632)]

 

Huenda Malaika hawa ndio wale wanaopandisha amali za waja kwa Allaah Ta’alaa.  Toka kwa Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy:

 

 "قَامَ فِينَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِخَمْسِ كَلِمَاتٍ فَقَالَ: "إِنَّ اللَّهَ عز وَجل لَا يَنَامُ وَلَا يَنْبَغِي لَهُ أَنْ يَنَامَ يَخْفِضُ الْقِسْطَ وَيَرْفَعُهُ يُرْفَعُ إِلَيْهِ عَمَلُ اللَّيْلِ قَبْلَ عَمَلِ النَّهَارِ وَعَمَلُ النَّهَارِ قَبْلَ عَمَلِ اللَّيْل"

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisimama baina yetu na kutuambia maneno matano:  Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Halali na haiwezekaniki Akalala, Anaishusha mizani na Anaipandisha, hupandishwa Kwake amali za usiku kabla ya amali za mchana, na amali za mchana kabla ya amali za usiku”.  [Muslim: (179)]

 

Allaah Ta’aalaa Ameipa utukuzo mkubwa Swalah ya Alfajiri.  Ametueleza kwamba Malaika Wake wanaihudhuria Swalah hii Aliposema:

 

"أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا"

 

Simamisha Swalaah jua linapopinduka hadi kiza cha usiku na Qur-aan ya (Swalaah ya) Alfajiri. Hakika Qur-aan ya Alfajiri ni yenye kushuhudiwa”.  [Al-Israa: 78]

 

 

Ibn Jariyr amesema:  “Qur-aan inayosomwa katika Swalah ya Alfajiri inakuwa ni yenye kushuhudiwa.  Wanaishuhudia Malaika wa usiku na Malaika wa mchana”.

 

 

Share