63-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (11)– Malaika Wanamfikishia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Salamu Toka Kwa Umma Wake Baada Ya Yeye Kufariki
Malaika
63: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini
(11)– Malaika Wanamfikishia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Salamu Toka Kwa Umma Wake Baada Ya Yeye Kufariki
Kumswalia na kumsalimia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni jambo lenye fadhla kubwa sana. Kati ya fadhla hizo, ni kwamba anayemsalimia Rasuli, basi salamu yake inamfikia moja kwa moja kaburini kwake, na salamu hiyo inafikishwa na Malaika maalum wenye kazi hiyo. Na hii ni katika mambo ya ghayb ambayo inabidi kama Waislamu tuyaamini.
Toka kwa ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhu): Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ لِلَّهِ مَلاَئِكَةً سَيَّاحِينَ فِي الْأَرْضِ يُبَلِّغُونِي مِنْ أُمَّتِي السَّلاَمَ"
“Hakika Allaah Ana Malaika Wake wanaozunguka ardhini, wananifikishia salamu toka kwa umma wangu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (1282) na Ahmad (3666)]
Hadiyth hii inatuhimiza tukithirishe kumswalia na kumsalimia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na inatubainishia namna Allaah Alivyomtukuza Nabiy Wake na kuienzi hadhi yake. Pia, inabainisha muujiza kati ya miujiza yake (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam).
Basi na tukithirishe kumswalia na kumsalimia Nabiy wetu (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam), na hii ni kwa faida yetu wenyewe.