64-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (12)– Malaika Wanawapa Habari Njema Waumini

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

64:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini

 

(12)– Malaika Wanawapa Habari Njema Waumini

 

Malaika huwapa Waumini habari njema itokayo kwa Allaah Ta’alaa.  Allaah Ta’alaa Anasema:

 

"إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ"

 

“Hakika wale waliosema:  Rabb wetu ni Allaah, kisha wakathibiti imara, Malaika huwateremkia (kuwaambia):  Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa”[Fus-swilat: 30]

 

As-Sam’aaniy amesema:  “Maneno haya huambiwa mtu wakati wa kufa, au wakati wa kufufuliwa”.

 

Abul ‘Aaliyah Ar-Riyaahiy amesema:  “Muumini atapewa habari ya furaha katika mahala patatu:  Wakati anaingia kaburini, wakati wa kufufuliwa, na wakati anaingia Peponi”.

 

Na katika baadhi ya Tafaasiyr, Mufassiruna wamesema:  “Mja akifufuliwa, watampokea Malaika wawili ambao walikuwa wanaandika amali zake na watamwambia:  Usiogope wala usihuzunike, bali pokea habari ya furaha ya kupata Pepo ambayo ulikuwa umeahidiwa, na wala yasikuogopeshe unayoyaona, hayo wamekusudiwa kwayo wengine”.

 

Hapa duniani, Malaika walimpa habari njema Nabiy Ibraahiym (‘alayhis salaam) ya kupata watoto wema.  Allaah Anatuambia:

 

"فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ"

 

Akawaogopa ndani ya nafsi yake.  Wakasema:  Usikhofu!  Na wakambashiria ghulamu mjuzi”.  [Adh-Dhaariyaat:  28]

 

Walimpa Zakariyaa pia habari njema ya kumpata Yahyaa (‘alayhimas salaam).  Allaah Anatuambia:

 

"فَنَادَتْهُ الْمَلَائِكَةُ وَهُوَ قَائِمٌ يُصَلِّي فِي الْمِحْرَابِ أَنَّ اللَّـهَ يُبَشِّرُكَ بِيَحْيَىٰ مُصَدِّقًا بِكَلِمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَسَيِّدًا وَحَصُورًا وَنَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ "

 

“Malaika akamwita (Zakariyyaa) naye akiwa amesimama anaswali katika chumba chake cha ‘ibaadah wakamwambia:  Hakika Allaah Anakubashiria Yahyaa atakayesadikisha Neno (la Kun!) kutoka kwa Allaah.  Atakuwa mtu wa kuheshimika, mtawa anayejitenga mbali na matamanio, na Nabiy miongoni mwa Swalihina”.  [Aal-‘Imraan: 39]

 

Habari hizi njema wanazotoa Malaika haziishilii kwa Manabii na Mitume tu, bali hata Waumini wengineo wanaweza kubashiriwa na Malaika.  Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أَنَّ رَجُلاً زَارَ أَخًا لَهُ فِي قَرْيَةٍ أُخْرَى، فَأَرْصَدَ اللَّهُ لَهُ عَلَى مَدْرَجَتِهِ مَلَكًا، فَلَمَّا أَتَى عَلَيْهِ قَالَ: أَيْنَ تُرِيدُ؟ قَالَ: أُرِيدُ أَخًا لِي فِي هَذِهِ الْقَرْيَةِ.‏ قَالَ: هَلْ لَكَ عَلَيْهِ مِنْ نِعْمَةٍ تَرُبُّهَا؟ قَالَ: لاَ، غَيْرَ أَنِّي أَحْبَبْتُهُ فِي اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ ‏.‏ قَالَ: فَإِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكَ بِأَنَّ اللَّهَ قَدْ أَحَبَّكَ كَمَا أَحْبَبْتَهُ فِيهِ"‏ 

 

“Kwamba mtu mmoja alimtembelea nduguye aliyekuwa mji mwingine.  Allaah Akamwekea njiani Malaika amngojee. Alipofika pale aliko Malaika, Malaika alimuuliza:  Unakwenda wapi?  Akamwambia:  Nimekusudia kuja kumwona ndugu yangu katika mji huu.  Akamuuliza:   Je, kuna maslahi yoyote kutoka kwake ambayo unayalinda?  Akasema hapana, hakuna chochote isipokuwa mimi nimempenda tu kwa ajili ya Allaah ‘Azza wa Jalla.  Akamwambia:  Basi mimi ni Mjumbe wa Allaah kwako, Amenituma nikueleze kwamba Allaah Amekupenda kama wewe ulivyompenda (nduguyo) kwa ajili Yake” .  [Swahiyh Muslim (2567)]

    

Hadiyth hii inatufundisha:

 

1-  Fadhila ya Waislamu kupendana kwa ajili ya Allaah na si kwa jingine lolote.

 

2- Kupendana na kutembeleana kwa ajili ya Allaah ni moja kati ya amali bora kabisa, na hasa ikiwa ziara bila ya maslahi yoyote ya kidunia.

 

 

Share