65-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (13)– Malaika Wanapigana Pamoja Na Waumini Na Wanawaimarisha Na Kuwatia Nguvu Vitani

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

 

65:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini

 

(13)– Malaika Wanapigana Pamoja Na Waumini Na Wanawaimarisha Na Kuwatia Nguvu Vitani

 

Allaah Ta’aalaa Amesema kuhusiana na watu wa Badri:

 

"إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ"

 

Pale Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia):  Hakika Mimi Niko pamoja nanyi; basi wathibitisheni wale walioamini.  Nitatia kizaazaa  katika nyoyo za waliokufuru.  Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kila kiungo (au ncha za vidole).   [Al-Anfaal: 12]

 

As-Sa’adiy akiifasiri aayah hii anasema:  “Allaah Ta’aalaa Aliwafunulia Malaika Wake kwa kuwaambia:  Hakika Mimi Niko pamoja nanyi kwa kuwapa msaada, nusra na kuwatieni nguvu, hivyo basi, wapeni uimara wale walioamini, yaani, tupieni katika nyoyo zao ushujaa wa kupambana na maadui zao, na wajazeni utashi wa kupigana Jihaad na kupupia fadhila zake”.

 

Allaah Ta’aalaa Ameelezea hikmah ya usaidizi huu wa Malaika kwa Waumini pale Aliposema: 

 

"وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ ۚ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ"

 

Na Allaah Hakujaalia haya isipokuwa ni bishara, na ili zitumainike nyoyo zenu kwayo.  Na hakuna nusura isipokuwa kutoka kwa Allaah.  Hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.  [Al-Anfaal: 10]

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema Siku ya Badr:

"هذا جِبريلُ آخِذٌ برأسِ فَرَسِه، عليه أداةُ الحَربِ"  

 

“Huyu ni Jibriyl, amekamata kichwa cha farasi wake, amevalia zana za kivita”.   [Swahiyh Al-Bukhaariy: (3995)]

 

Hapa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwazindusha Maswahaba wake juu ya uwepo wa Jibriyl katika uwanja wa vita ili kuwapa ukakamavu, uimara na morali zaidi, lakini pia kuwatuliza nyoyo. 

 

Katika Vita vya Badr, baadhi ya Maswahaba walisikia kishindo cha pigo la Malaika kwa kafiri.  Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema:

 

"بَيْنَمَا رَجُلٌ مِنَ الْمُسْلِمِينَ يَوْمَئِذٍ يَشْتَدُّ فِي أَثَرِ رَجُلٍ مِنَ الْمُشْرِكِينَ أَمَامَهُ، إِذْ سَمِعَ ضَرْبَةً بِالسَّوْطِ فَوْقَهُ وَصَوْتَ الْفَارِسِ يَقُولُ: أَقْدِمْ حَيْزُومُ ‏.‏ فَنَظَرَ إِلَى الْمُشْرِكِ أَمَامَهُ فَخَرَّ مُسْتَلْقِيًا فَنَظَرَ إِلَيْهِ فَإِذَا هُوَ قَدْ خُطِمَ أَنْفُهُ وَشُقَّ وَجْهُهُ كَضَرْبَةِ السَّوْطِ فَاخْضَرَّ ذَلِكَ أَجْمَعُ ‏.‏ فَجَاءَ الأَنْصَارِيُّ فَحَدَّثَ بِذَلِكَ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ ‏"‏ صَدَقْتَ ذَلِكَ مِنْ مَدَدِ السَّمَاءِ الثَّالِثَةِ ‏"

 

“Katika siku hiyo, wakati Muislamu alipokuwa anamkimbiza mpagani aliyekuwa anakimbia mbele yake, ghafla alisikia sauti ya pigo la mjeledi juu yake na sauti ya mpanda farasiakisema:  Ongeza mbio Khayzuwm. Akamwangalia mpagani akamwona anaanguka chali mbele yake, na alipomkagua vizuri, aliona pua ina kovu na uso wake umepasuliwa kama vile amepigwa na mjeledi, huku mwili wake wote ukiwa umegeuka kijani.  M-Answaariy huyo alikwenda na kulielezea tukio kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Rasuli akamwambia:  Umesema kweli, huyo alikuwa (Malaika wa) msaada toka mbingu ya tatu”.  [Swahiyh Muslim: (1763)]

 

Khayzuwm ni jina la farasi wa Malaika huyo.

 

Kadhalika, katika Vita vya Makundi, Siku ya Khandaq, Jibriyl pia aliwasaidia Waumini.  Bibi ‘Aaishah amesema:

"فَلَمَّا رَجَعَ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم مِنَ الخَنْدَقِ وَضَعَ السِّلَاحَ، فَاغْتَسَلَ، فأتَاهُ جِبْرِيلُ وَهو يَنْفُضُ رَأْسَهُ مِنَ الغُبَارِ، فَقالَ: وَضَعْتَ السِّلَاحَ؟ وَاللَّهِ ما وَضَعْنَاهُ، اخْرُجْ إليهِم، فَقالَ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم: فأيْنَ؟ فأشَارَ إلى بَنِي قُرَيْظَةَ، فَقَاتَلَهُمْ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فَنَزَلُوا علَى حُكْمِ رَسولِ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فَرَدَّ رَسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم الحُكْمَ فيهم إلى سَعْدٍ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliporejea toka Vita vya Khandaq, aliirejesha silaha yake mahala pake, kisha akaoga.  Jibriyl akamjia huku akikun’guta vumbi kichwa chake.  Akamuuliza:  Umeweka silaha chini?  Naapa kwa Allaah, sisi bado hatujaweka silaha chini, toka uwafuate.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:  Wapi? Akamwashiria kwenda kwa Baniy Quraydhwah.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akapambana nao mpaka wakasalimu amri kuwa chini ya utawala wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaurejeshea utawala kwa Sa’ad awaongoze”.   [Al-Bukhaariy (4122) na Muslim (1769)]

 

Haya yote yanaonyesha kwamba Malaika huandamana na wanaopigana katika Njia ya Allaah, na huwasaidia madhali watakuwa ni wenye kufuata Maagizo ya Allaah na Rasuli Wake, na kama watakwenda kinyume nayo, basi hapo hufarikiana na kuachana nao.

 

 

 

Share