71-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (19)– Malaika Wanawateremshia Makafiri Adhabu

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

71:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini  

 

(19)– Malaika Wanawateremshia Makafiri Adhabu

 

Kama tunavyosoma katika Qur-aan Tukufu, Allaah Ta’aalaa Aliwaangamiza watu ambao waliwakadhibisha Mitume wao, na kazi ya kuwaangamiza ilikuwa inafanywa na Malaika katika baadhi ya nyakati.  Mfano kaumu Lut, Allaah Ta’alaa Anatuambia:

 

"فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ"

 

Basi ilipokuja Amri Yetu, Tuliupindua (mji wao) juu chini, na Tukauteremshia mvua mfululizo ya mawe ya udongo mgumu uliookwa”.  [Hud: 82]

 

Jibriyl ‘Alayhis Salaam ndiye aliyefanya kazi hii.

 

Wakati wa kutoka roho kwa makafiri, Malaika pia hufanya kazi ya kuwaadhibu.  Allaah Anatuambia:

 

"وَلَوْ تَرَىٰ إِذِ الظَّالِمُونَ فِي غَمَرَاتِ الْمَوْتِ وَالْمَلَائِكَةُ بَاسِطُو أَيْدِيهِمْ أَخْرِجُوا أَنفُسَكُمُ ۖ الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ عَذَابَ الْهُونِ بِمَا كُنتُمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ وَكُنتُمْ عَنْ آيَاتِهِ تَسْتَكْبِرُونَ"

 

"Na lau ungeliona madhalimu pale wakiwa katika mateso makali ya mauti (ungeona jambo la kutisha sana), na Malaika wamenyosha mikono yao (wakiwaambia):  Toeni nafsi zenu!  Leo mnalipwa adhabu ya kudhalilisha kwa yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Allaah pasi na haki, na mlikuwa mkitakabari msizifuate Aayaat Zake”.   [Al-An’aam: 93]

 

Halafu kaburini, kuna Malaika wawili Munkar na Nakiyr.  Hawa watawatahini wafu na kuwauliza maswali, na atakayeshindwa kujibu, basi ole wake.

 

Kisha Siku ya Qiyaamah, Malaika watawaswaga watu wa motoni na kuwakabidhi kwa walinzi wa moto ambao watawaadhibu na kuwatesa ndani ya moto wa Jahannam.  Allaah Atulinde nao.

 

 

Share