72-Malaika: Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini: (20)– Malaika Wanawalaani Makafiri na Baadhi Ya Watu Mafasiki

 

Malaika

 

Alhidaaya.com

 

72:   Nafasi Ya Malaika Kwa Waumini  

 

(20)– Malaika Wanawalaani Makafiri na Baadhi Ya Watu Mafasiki

 

Allaah Ta’aalaa Anatuambia:  

 

"إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ لَعْنَةُ اللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ "

 

“Hakika wale waliokufuru na wakafa hali ya kuwa ni makafiri, hao iko juu yao Laana ya Allaah na Malaika na watu wote”.  [Al-Baqarah: 161]

 

Malaika hawalaani makafiri tu, bali pia wanawalaani Waislamu ambao wamefanya madhambi maalum.  Kati ya watu hao ni:

 

1-  Mwenye kuficha haki:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ "

“Hakika wale wanaoficha yale Tuliyoyateremsha katika hoja bayana na mwongozo baada ya kuwa Tumeyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao Anawalaani Allaah na wanalaaniwa na kila mwenye kulaani”.  [Al-Baqarah: 159] 

 

Ibn Al-Jawziy amesema:  “Kuna kauli nne kuhusiana na wenye kumlaani mtu huyu:

 

Ya kwanza:  Ni wanyama wa ardhini.  Ya pili:  Ni Waumini.  Ya tatu:  Ni Malaika na Waumini.  Ya nne:  Ni majini, wanadamu na wanyama wote”.

 

Ama As-Sa’adiy, yeye kasema:  “Ni viumbe wote wanamlaani, laana toka viumbe wote inawateremkia.  Kwa kuwa watu hawa lengo lao kuu ni kudanganya watu, kuharibu dini yao na kuwaweka mbali na Rahma ya Allaah.  Hivyo wanalipwa kwa mujibu wa matendo yao”.   

 

Kama ambavyo mtu mwenye kuwafundisha watu kheri, Allaah pamoja na Malaika Wake Humsalia mtu huyo, hadi samaki ndani ya maji, kwa kuwa mtu huyo lengo lake kuu ni maslaha ya viumbe, kuwatengenezea dini yao, na kuwakurubisha kwenye Rehma za Allaah.  Hivyo naye analipwa kwa mujibu wa lengo na juhudi zake hizo.

 

2-  Mwanamke asiyemwitikia mumewe kwa tendo la ndoa: 

 

Abu Hurayrah amesema:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِذَا دَعَا الرَّجُلُ امْرَأَتَهُ إِلَى فِرَاشِهِ فَأَبَتْ فَبَاتَ غَضْبَانَ لَعَنَتْهَا الْمَلَائِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ"

 

“Mume akimwita mkewe kitandani halafu akakataa, na mume akalala hali ya kuwa amemkasirikia, basi Malaika watamlaani hadi kupambazuke”.  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Malaika humlaani kwa sababu mwanamke ameamuriwa amtii mumewe kwenye jambo lolote lisilo la maasia isipokuwa kama kuna udhuru.  Na hedhi si udhuru wa kumkatalia, kwa kuwa mume ana haki ya kumchezea sehemu zote za mwili isipokuwa utupu.  Na hukmu ya mchana ni hivyo hivyo, watamlaani mpaka jua lichwe.

 

Ibn ‘Uthaymiyn amesema:  “Laana ya Malaika ina maana kwamba wanamwombea laana mwanamke huyu, na laana ni kuwekwa mbali na Rahma ya Allaah”.

 

3-  Mwenye kumnyooshea nduguye kipande cha chuma (au silaha):

 

 Abu Hurayrah amesema:  "Abul Qaasim (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ أَشَارَ إِلَى أَخِيهِ بِحَدِيدَةٍ فَإِنَّ الْمَلَائِكَةَ تَلْعَنُهُ حَتَّى يَضَعَهَا وَإِنْ كَانَ أخاهُ لأبيهِ وَأُمِّهِ"

 

“Atakayemnyooshea nduguye chuma (au silaha), Malaika watakuwa ni wenye kumlaani mpaka aiweke chini, hata kama ni nduguye wa baba na mama mmoja”.  [Swahiyh Muslim: 2616]

 

Kunyooshea huku ni sawa kuwe kwa utani au kukusudia kikweli.

 

4-  Mwenye kuzusha au kufanya lolote baya Madiynah:

Abu Hurayrah amesimulia:

 

"الْمَدِينَةُ حَرَمٌ، فَمَنْ أَحْدَثَ فِيهَا حَدَثًا أَوْ آوَى مُحْدِثًا فَعَلَيْهِ لَعْنَةُ اللَّهِ وَالْمَلاَئِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ، لاَ يُقْبَلُ مِنْهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَدْلٌ وَلاَ صَرْفٌ"

 

“Madiynah ni takatifu yenye marufuku maalum.  Basi yeyote atakayezusha humo lisilo katika dini, au akampa hifadhi mzushaji, basi zimpate laana za Allaah, Malaika na watu wote.  Hatokubaliwa Siku ya Qiyaamah fidia wala toba”.   [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Share