73-Malaika: Wanachopaswa Waumini Kukitenda Kwa Ajili Ya Malaika: (01)- Kujiepusha Na Kila Jambo Linalowaudhi Au Kuwakera
Malaika
73: Wanachopaswa Waumini Kukitenda Kwa Ajili Ya Malaika
(01)- Kujiepusha Na Kila Jambo Linalowaudhi Au Kuwakera
Waumini wanatakiwa kujiepusha na kila jambo ambalo linawakera au kuwaudhi Malaika. Jambo kubwa linalowakera zaidi ni ukafiri, shirki, madhambi na maasia. Na kwa ajili hiyo, Malaika hawaingii nyumba ambazo ndanimwe kuna watu wanaomwasi Allaah, au nyumba ambazo ndanimwe kuna Anayoyachukia Allaah kama masanamu na picha. Vile vile, hawamkurubii mtu aliyevaana na maasia kama mlevi, mraibu na kadhalika.
Toka kwa Abu Twalha Al-Answaariyy (Radhwiya Allaah ‘anhu): “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لا تَدْخُلُ الْمَلاَئِكَةُ بَيْتًا فِيهِ كَلْبٌ وَلاَ صُورَةٌ "
“Malaika (wa rahmah na baraka) hawaingii nyumba yoyote ambamo ndani yake kuna mbwa au picha”. [Sunan An Nasaaiy (5347)]
Toka kwa ‘Abdullah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa):
"ثَلَاثٌ لَا تَقْرَبُهُمُ الْمَلَائِكَةُ: جِيفَةُ الْكَافِرِ، وَالْمُتَضَمِّخُ بِالْخَلُوقِ، وَالْجُنُبُ إِلَّا أَن يتَوَضَّأ"
“Malaika (wa rahma) hawawakurubii watatu: Mzoga wa kafiri, aliyejisiriba khaluwq, na mwenye janaba mpaka atawadhe”. [Swahiyh At-Targhiyb: 174]
“Khaluwq” ni aina ya manukato yenye rangi, hutengenezwa kutokana na zafarani na mada nyinginezo.
Kadhalika, Malaika hawawakurubii watu wenye kengele. Abu Hurayrah amesema: (Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا تَصْحَبُ الْمَلَائِكَةُ رُفْقَةً فِيهَا كَلْبٌ وَلَا جَرَسٌ"
“Malaika hawaandamani na wasafiri wenye mbwa au kengele”. [Mishkaat Al-Maswaabiyh: (3894)]
Jingine linalowakera na kuwaudhi Malaika ni kila chenye kuwaudhi na kuwakera wanadamu kama harufu mbaya, uvundo, uchafu na kadhalika.
Toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu): “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ أَكَلَ الْبَصَلَ وَالثُّومَ وَالْكُرَّاثَ فَلاَ يَقْرَبَنَّ مَسْجِدَنَا، فَإِنَّ الْمَلاَئِكَةَ تَتَأَذَّى مِمَّا يَتَأَذَّى مِنْهُ بَنُو آدَمَ "
“Aliyekula kitunguu maji, au kitunguu thawm, au kitunguu majani, basi akae mbali kabisa na Msikiti wetu, kwa kuwa Malaika wanakereka na yale yanayowakera watu”. [Muslim 564]
Kadhalika, Muislamu anaposwali, asiteme upande wake wa kulia. Hilo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelikataza. Kwa kuwa mtu anaposwali, Malaika husimama upande wake wa kulia.
Toka kwa Abu Hurayrah: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا قَامَ أَحَدُكُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَلَا يَبْصُقْ أَمَامَهُ فَإِنَّمَا يُنَاجِي اللَّهَ مَا دَامَ فِي مُصَلَّاهُ، وَلَا عَنْ يَمِينِهِ فَإِنَّ عَنْ يَمِينِهِ مَلَكًا، وَلْيَبْصُقْ عَنْ يَسَارِهِ أَوْ تَحْتَ قَدَمِهِ فَيَدْفِنُهَا"
“Anaposimama mmoja wenu kuswali, basi asiteme mbele yake, kwa sababu anakuwa ni mwenye kusemezana na Allaah madhali yuko sehemu yake anayoswalia. Na pia asiteme kuliani mwake, kwani kuliani mwake yuko Malaika. Ateme kushotoni mwake, au chini ya mguu wake, halafu afukie. [Al-Bukhaariy na Muslim]