03-Tukumbushane: Mali Ni Niqama
Tukumbushane
03: Mali Ni Niqama:
Mali mbali na kuwa ni neema toka kwa Allaah, pia inakuwa ni naqama. Inaweza kuwa ndio sababu kubwa ya kumweka mbali mtu na Allaah na kuwa kitendakazi cha nguvu cha kumsahaulisha na aakhirah kama hali ya mambo tunavyoiona hivi leo. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam anasema:
"إِنَّ لِكُلِّ أُمَّةٍ فِتْنَةٌ وَإِنَّ فِتْنَةَ أُمَّتِي الْمَالُ"
“Hakika kila umma una mtihani wake, na hakika mtihani wa umma wangu ni mali”.
Uchu na ulafi wa mwanadamu kwa mali hauna mipaka hata akiwa na mabonde mawili ya dhahabu angelitamani awe na la tatu. Uchu huu mbaya unamsukuma kutafuta mali kwa njia yoyote ile iwayo hata ya haramu. Na ikiwa chumo litakuwa la haramu, basi tabaka za nyama za haramu zitaendelea kumea kwenye mwili, na zikifikia kumea kikamilifu, basi zitasubiriwa na moto wa Jahannam uzisafishe. Rasuli anasema:
"لَا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ لَحْمٌ نَبَتَ مِنْ سُحْتٍ ، النَّارُ أَوْلَى بِهِ"
“Haiingii Peponi nyama iliyomea kutokana na haramu, na Moto unaistahikia zaidi”. [Imesimuliwa na Ahmad toka kwa Jaabir. Isnadi yake ni Jayyid]
Askari wa usalama barabarani wanaokusanya kila siku hongo za mamilioni toka kwa madereva, watumishi wa serikali na wengineo wengi walio kwenye nafasi zao, au waporaji wa mali za umma, hao wote miili yao inanona kwa pesa ya haramu, na wajue kuwa moto wa Jahannam utazipaparikia zaidi nyama zao. Ni furaha ya muda mfupi tu waliyonayo, lakini majuto ni marefu yasiyo na ukomo. Usiombee kuwa katika nafasi hizo, au mtoto wako, au Muislamu mwenzako.