05-Tukumbushane: Ulimi Ni Neema

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

05:  Ulimi Ni Neema:

 

 

Ulimi ni kiungo pekee katika mwili wa mwanadamu ambacho hakichoki vyovyote kitakavyofanya kazi.  Na hii ni moja kati ya Fadhila za Allaah kwetu ili tuweze kuvuna zaidi matunda ya Peponi kwa adhkaar, kusoma Qur-aan na kunena maneno mema, maneno ya haki na kadhalika.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:

 

"مَنْ قَالَ (سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِحَمْدِهِ) غُرِسَتْ لَهُ نَخْلَةٌ فِي الْجَنَّةِ"

 

“Mwenye kusema: Subhaana Allaah Al-‘Adhwiym wa bihamdihi, atapandiwa mtende Peponi”.  [Swahiyh At-Targhiyb.  Swahiyh Lighayrih]

 

Ni vidole vingapi vitaumwa kwa majuto kwa mitende iliyopotezwa na watu Peponi kwa kushindwa tu kutamka maneno machache kama hayo na mengineyo mengi ya kheri kwa kushughulishwa na mambo yasiyo na faida yoyote?!  Ni urahisi ulioje wa kuyatamka maneno kama haya!  Hayana wakati maalum, wala sehemu maalum, wala nyenzo maalum wala masharti maalum.  Ni kwa ulimi wako tu ambao hauhisi tabu yoyote vyovyote utakavyounenesha.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema tena:

 

"ليسَ يتحسَّرُ أَهلُ الجنَّةِ على شيءٍ إلَّا على ساعَةٍ مرَّت بِهِم لم يذكُروا اللَّهَ عزَّ وجلَّ فيها" 

 

“Hakuna kitu ambacho watu wa Peponi watakijutia zaidi kuliko saa moja iliyowapitia bila ya kumdhukuru Allaah ‘Azza wa Jalla ndani yake”.  [Hadiyth Hasan.  Al-Jaami’u As Swaghiyr]

 

Hawa ni watu wa Peponi.  Je wa motoni majuto yao yatakuwa vipi?!  Tuzindukane na wakati wetu.

                                                              

 

Share