07-Tukumbushane: Jicho Ni Neema

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

07:  Jicho Ni Neema:

 

 

Allaah Ameliumba jicho ili liwe ni moja ya macho mawili aliyoyakusudia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika neno lake:

 

"عَينانِ لا تمسُّهُمَا النَّارُ: عَينٌ بَكَتْ مِنْ خَشْيَةِ اللَّهِ، وعَينٌ بَاتَتْ تحرُسُ فيْ سِبِيْلِ اللَّهِ

 

“Macho mawili moto hautoyagusa:  Jicho lililotokwa na machozi kwa kumkhofu Allaah, na jicho lililokesha usiku likichunga katika Njia ya Allaah”.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposema:  Macho mawili hayaguswi na moto”, anamaanisha aina mbili za watu ambao hawataingia motoni.  Amewaelezea kwa jicho ili kuashiria kwamba viungo vingine vya mwili vinastahiki zaidi visiadhibiwe kwa moto.

 

Ama jicho linalolia kwa kumkhofu Allaah, hili ni lile la mtu anayetokwa na machozi kwa sababu ya khofu na matarajio kwa Allaah ‘Azza wa Jalla wakati anapotubia, au anapomdhukuru Allaah, au anapofanya jambo jema la utiifu kwa Allaah.  Na hii ni Rahma jumla kwa kila Muislamu anayesifika kwa sifa hii.

 

Ama jicho linalokesha katika Njia ya Allaah, hili ni lile linalowalinda Waislamu wasije kushambuliwa ghafla na maadui katika Vita vya kulinyanyua juu Neno la Allaah, au linalokesha kwa ajili ya Hajji, au kutafuta ilmu, au kusaidia wanyonge, au kuwatetea wadhulumiwa na wanyonge na mfano wa hayo katika ibada zote zinazohitajia juhudi na uzito katika kuzifanikisha.

 

Allaah Ta’aalaa Ameliumba jicho pia ili mtu aweze kutafakuri kwa anayoyaona katika Uumbaji wa Allaah na kuzunguka nalo katika Ufalme Mkubwa wa Allaah ili iymaan ya Muislamu izidi kukua na yaqini izidi kuimarika hadi kujikuta akisema mwenyewe:

 

"رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ"

 

Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako, basi Tukinge na adhabu ya moto”.

                                                             

 

 

Share