09-Tukumbushane: Wakati
Tukumbushane
09: Wakati:
Wakati ni neema. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza:
"نِعْمَتانِ مَغْبُونٌ فِيهِما كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ: الصِّحَّةُ والفَراغُ"
“Neema mbili watu wengi wamekula hasara ndani yake: afya na faragha”. [Al-Bukhaariy]
Watu wengi wanapoteza afya na wakati wao wa faragha bila faida. Hawaitumii neema hiyo kwa yenye kuwafaa, wala yenye kuwakurubisha kwa Allaah, na wala yenye kuwafaa wao na wengineo kwenye dunia yao. Watu hawa wanakuwa ni wenye kujipunja wenyewe ndani ya neema hizi na kujidhulumu, na hii ni hasara kubwa.
Hadiyth hii inatuashira kwamba mtu hawezi kuwa na nafasi nzuri ya kufanya matendo mema ila atakapokuwa ana cha kumtosheleza mahitaji yake, yupo kwenye amani, na ana afya njema. Anaweza kuwa anajitosheleza lakini mgonjwa, au ana afya nzuri lakini hana cha kutosheleza mahitaji yake ya kimsingi, au kuna mengi ya kumtatiza kama kukosekana usalama, amani na kadhalika. Katika hali hii, anakuwa ni mwenye kushughulishwa na matibabu au kusaka tonge, na akili na hima yake yote inajikita katika kujinasua na hali aliyonayo, hivyo muda wa kuzingatia ibada njema unakuwa haupo.
Lakini pia kuna mtu anaweza kuwa anamiliki cha kumtosha vizuri, afya njema na usalama, pamoja na hivyo asiutumie vyema wakati wake wala afya yake. Huyu ndiye mkusudiwa wa Hadiyth hii. Atakuwa anajipunja na kujihasiri mwenyewe kwa kupoteza nafasi hiyo bure. Wakati wa kufa atakapoona hasara ya hilo, au Siku ya Qiyaamah, atajuta sana atakapoona daftari lake limesajili muda wake mwingi kuwa aliutumia kwenda viwanja vya mipira, kufuatilia ligi kuu za ndani na nje na kadhalika, wakati madaftari ya wengine yamejaa adhkaar, visomo vya Qur-aan, mahudhurio ya mihadhara ya kidini na mengineyo nufaishi na kadhalika. Muislamu asisubiri majuto hayo, bali aharakie na kuchukua hatua ya haraka ya kuupanga wakati wake vizuri katika mambo ya kheri na ya kumfaa yeye mbele ya safari ndefu na nzito huko Aakhirah.