11-Tukumbushane: Nabiy Ibraahiym Atakataliwa Uombezi Wake Kwa Baba Yake Siku Ya Qiyaamah

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

11:  Nabiy Ibraahiym Atakataliwa Uombezi Wake Kwa Baba Yake Siku Ya Qiyaamah:

 

Abu Hurayrah:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) atakutana na baba yake Aazar Siku ya Qiyaamah uso wake ukiwa umejaa vumbi umesawijika.  Ibraahiym atamwambia: Je sikukwambia kwamba usikatae maneno yangu na usia wangu?!  Baba yake atamjibu:  Leo mimi sitokuasi.  Ibraahiym atasema:  Ee Rabbi wangu!  Hakika Wewe Umeniahidi kuwa Hutonikhizi Siku watu watakapofufuliwa.  Basi ni khizaya iliyoje baba yangu kuwa mbali kabisa (na Rahmah za Allaah)?!  Allaah Ta’aalaa Atamwambia:  Hakika Mimi Nimepiga marufuku Pepo kwa makafiri. Kisha patasemwa:  Ee Ibraahiym!  Angalia chini ya miguu yako, naye ataangalia. Hapo atashtukizwa kumwona fisi aliyetapakaa damu.  Fisi atakamatwa miguu na mikono yake atupwe motoni”.  [Swahiyh Al-Bukhaariy.  Imesimuliwa na Abu Hurayrah]

 

Allaah Mtukufu Ameiharamisha Pepo kwa makafiri.  Yeyote anayekufa kafiri, basi moto wa milele unamsubiri.  Hii ni Ahadi ya Allaah, hakuna uombezi utakaomfaa Siku hiyo wala nasaba. Na hapa tunaona namna ambavyo Ibraahiym anajaribu kumwomba Allaah Asimkhizi kama Alivyomwahidi ili Amsamehe baba yake na Amwingize Peponi.  Na kwa kuwa baba huyo alikufa kafiri baada ya kukataa hoja zote za wazi alizoletewa na mwanawe juu ya ujinga wa kuabudu masanamu yasiyosikia wala kuona, wala kunufaisha wala kudhuru, na juu ya msingi huo wa ukafiri, Atamkatalia kuingia Peponi.  Na badala yake Atamgeuza kuwa fisi aliyetapakaa damu na kuwa katika picha ya kukirihisha na atupwe motoni ili Ibraahiym  asiwe na hamu naye tena na ajivue naye kabisa.

 

Tunajifunza hapa kwamba:

 

1-   

 Mtoto Muislamu hatoweza kumsaidia mzazi wake kafiri Siku ya Qiyaamah hata kama mtoto ni Nabiy.

 

2-   

 Tujitahidi kuulinda Uislamu wetu kwa nguvu zote ili tufe nao.  Kuulinda ni kujitahidi kuwajibika na yote Aliyoyaamuru Allaah, kujiepusha na yote Aliyoyakataza na kumcha Allaah wakati wote na mahala pote.

 

 

Share