14-Tukumbushane: Faida Ya Hofu Na Huzuni Hapa Duniani

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

14:  Faida Ya Hofu Na Huzuni Hapa Duniani:

 

Hofu ni hisia ya kuogopa jambo lijalo ambalo bado halijatuka, na huzuni ni hisia itokanayo na jambo lililopita.  Mwanadamu hapa duniani anahofia riziki yake, anajihofia mwenyewe, anahofia watu wake, kudhulumiwa, kunyanyaswa, mauti, kifo, umasikini na kadhalika.  Pamoja na haya yote, anaweza kuhuzunika kwa kufiwa na mwanaye, au kukosa ajira, kukosa mtoto na misiba mingineyo ya maisha.  Haya yote ni katika misukosuko ya maisha ya hapa duniani.  Na misukosuko hii haipiti bure, bali inatupandishia daraja, na inatububujishia Rahma na Baraka kochokocho toka kwa Allaah.  Na hii ni kwa muumini mwenye subira tu.

 

Na kutokana na hofu na huzuni tunazozipata hapa duniani, tutakapoingia Peponi, hapo ndipo tutakapohisi ladha halisi ya amani na furaha ya huko.  Mtu hawezi kuhisi ladha ya shibe bila kupata adha ya njaa kali.  Hatuwezi kuhisi ladha ya amani na usalama bila kuonja makali ya ukosefu wa amani.

 

Na huko pia, hakuna mitihani wala misukosuko kwa Waumini wema, bali ni mabubujiko ya Rahma na Radhi za Allaah ambazo zitaondosha kabisa hofu kubwa itakayotanda Siku ya Qiyaamah.  

                               

Share