16-Tkumbushane: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Viumbe?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

16:  Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Viumbe?

 

Viumbe vyote vinamsabbih Allaah na wala havichoki; wanyama, mimea, majini, Malaika, bahari, milima, mabonde na kadhalika.  Allaah Anatuambia:

 

"وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ"

 

“Na hakuna kitu chochote (kile kiwacho) isipokuwa kinasabihi kwa Himidi Zake, lakini hamzifahamu tasbiyh zao”.  [Al-Israa 44]

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam anatuambia:

 

"إنَّ اللهَ أذِنَ لي أن أُحدِّثَ عن ديكٍ قد مَرَقَتْ رجلاه الأرضَ، وعُنُقُه مَثْنِيَّةٌ تحت العرشِ، وهو يقول: سبحانك ما أعظَمك! فيردُّ عليه: لا يعلم ذلك من حلفَ بي كاذبًا "

 

“Hakika Allaah Amenipa idhini nimzungumzie jogoo ambaye miguu yake miwili imepenya kuingia ardhini, na shingo yake imeinamishwa chini ya ‘Arshi, naye anasema: Umetakasika.  Ni Uadhwama na Ukubwa ulioje Wako (ee Allaah)! Allaah Humjibu: Halijui hilo mwenye kuapa kwa uongo kwa Jina Langu”. [Swahiyh Al-Jaamiu.  Al-Albaaniy:  Ni Swahiyh]

 

Huyo ni jogoo wa ukubwa huo anayemsabbih Allaah.   Vipi ukubwa wa Allaah Aliyemuumba!  Hilo watu wangelijua, basi wasingelithubutu kuapa kwa uongo na kuchezea Jina la Allaah Mwenye ukubwa na uadhwama usioweza kufikirika. Jogoo huyu baadhi ya Maulamaa wanasema ni katika wale Malaika wanane wabebao ‘Arshi ya Allaah, na yuko katika umbile la jogoo.  Na hao Malaika wabebaji ‘Arshi, kutoka kwenye njewe ya sikio hadi bega lake ni safari ya mwendo wa miaka 700 kwa ndege kupiga mbawa zake.   Jibril ‘alayhis salaam ana mbawa 600 zinazofunika mashariki yote ya uso wa dunia, naye pia pamoja na hao Malaika na wengineo, hachoki kumsabbih Allaah nyakati zote.  Kwa picha hii, tunapata kujua fadhla kubwa ya kumsabbih Allaah.

 

Kwa nini iwe tasbiyh pekee inayotamkwa na viumbe vyote badala ya adhkaar nyingine?   Hakika iko siri kubwa ndani yake.

 

Ikiwa viumbe hivyo vikubwa vinamsabbih Allaah bila kuchoka, mnyama unayempanda, nguo unazozivaa, kiti unachokalia, na hata udongo unaoukanyaga, au wadudu unaowadharau na kuwatweza kama nzi na kadhalika,  je, huoni haya wewe kuwa nje ya duara la wanaomsabbih Allaah na kushindwa na hata viumbe wadogo kabisa!

Jitafakuri na jiweke sawa.

 

 

Share