17-Tukumbushane: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Malaika?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

17:  Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Malaika?

 

Waonee haya Malaika wawili wanaoandamana nawe nyakati zote kwa ajili ya kuandika matendo yako yote madogo au makubwa; mema au mabaya.  Matendo yako ya mchana hupandishwa kabla ya kuingia usiku, na ya usiku kabla ya kuingia siku mpya.  Je, unaridhia rekodi ya matendo yako yanayopandishwa kuwa ni dhambi tupu? Hujisikii vibaya?!

 

Hebu jaribu kufanya kama unawaona wanavyosajili matendo yako!  Fanya kama unamwona Malaika wa kuumeni anavyoandika matendo yako mema, na wa kushotoni anavyoandika kila dhambi lako.  Jaribu kuwaza kwa kina, utakuwa unajisikiaje ukiona mema yako yanasajiliwa dogo lake na kubwa lake hata la uzito wa sisimizi bila ya Malaika huyo kuchelewa hata sekunde moja?  Nadhani ukiikita picha hiyo kiuhalisia, hutozembea hata kidogo kujiongezea mema nyakati zote. Hali kadhalika kwa mabaya, utajikuta ukichukua hadhari kubwa kwa kila tendo unalotaka kulifanya au neno unalotaka kulitamka.  Lakini huo ndio ukweli na uhalisia wa mambo.

 

Kwa dereva wa gari aliyepigwa tochi na askari wa usalama na kuletewa sms ya kulipa faini, huyu faini hii itamtesa sana kabla ya kulipa na hata baada ya kulipa. Hawezi kuisahau!  Ni kama kidonda.  Sasa hali ikoje kwa madhambi tunayoyachuma kila wakati huku tukisahau kabisa kama yanarekodiwa hapo kwa papo na kuhifadhiwa, na tutakuja kuyaona siku ya hisabu?  Haya pia yatatutesa sana tutakaposimama mbele ya Allaah kwa ajili ya hisabu hiyo, isipokuwa kama tutatubia yakafutwa na kuondoshwa.

 

Allaah Anatuambia:

 

"وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا"

 

“Na kitawekwa Kitabu, basi utaona wakhalifu ni wenye khofu kwa yale yaliyomo ndani yake; na watasema:  Ole wetu!  Kitabu hiki kina nini? Hakiachi dogo wala kubwa isipokuwa kimerekodi hesabuni.  Na watakuta yale waliyoyatenda yamehudhuria hapo.  Na Rabb wako Hamdhulumu yeyote”.  [Al-Kahf: 49]

 

 

Piga hesabu sahihi ndugu yangu kabla ya kufanya tendo lolote, na kabla ya kutamka lolote.  Kama ni la kheri, basi lifanye, na kama ni la shari, basi achana nalo.  Inatosha tu kujua kwamba uko na Malaika hao wawili wanakuona na kusajili, Allaah Anakuona vizuri tu, na viungo vyako vinakuona na hata ardhi pia. Jisikie haya ufaulu duniani na aakhirah.

                                                             

 

Share