18-Tukumbushane: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Mtu Mwema Katika Jamaa Zako?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

18:  Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Mtu Mwema Katika Jamaa Zako?

 

Abu Sa’iyd Al-Azdiy alimwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) niusie.  Rasuli akamwambia: 

 

"أُوصِيكَ أَنْ تَسْتَحِيَ مِنَ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ كَمَا تَسْتَحِي مِنَ الرَّجُلِ الصَّالِحِ"

 

“Ninakuusia umwonee haya Allaah ‘Azza wa Jalla kama unavyomwonea haya mtu mwema”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As Swahiyhah 741]

 

Ndugu yangu Muislamu!

 

Hebu chukulia kwamba mtu mwema katika jamaa zako ameshukia nyumbani kwako kama mgeni wako, kisha akakuomba uswali naye pamoja hapo nyumbani. Je, hali yako itakuwaje ikiwa wewe huswali?!  Au, acha hilo, akakutaka msome pamoja Qur-aan hali ya kuwa Msahafu wako umejaa vumbi hujaugusa tena tokea Ramadhani iliyopita!  Au akakutaka umwonyeshe Msikiti wa karibu ilhali wewe daima umejitupa kwenye kochi lako, unasikia adhana na wala huendi kuswali na pengine hata Msikiti hujui ulipo.  Au akataka kuswali hapo nyumbani akakutaka umwelekeze Qiblah nawe hujui kilipo!   Fikiria hali yako itakuwaje au jibisho lako?!  Ni fedheha tupu!!

 

Bila shaka katika hali hii, kwa kumwonea haya mtu huyu, kuchunga hisia zake na wewe mwenyewe kujisitiri asikujue tabia yako hiyo, kwa kutahayari, utajikuta unaswali naye hivyo hivyo.  Na hapa inaingia shirki ndogo ya riyaa, na wewe mwenyewe unakuwa umejiingiza humo kwa mikono yako miwili.  Na hii pia ni katika sifa za wanafiki Allaah Atulinde nayo.

 

Ikiwa kwa binadamu huyu unalazimika kufanya hivyo, basi iko wapi hisia yako ya haya kwa Allaah Anayejua mambo yako yote na Anakuona unavyopuuza Maamrisho Yake?!

 

 

 

Share