19-Tukumbushane: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Allaah ‘Azza Wa Jalla?
Tukumbushane
19: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Allaah ‘Azza Wa Jalla?
Inakutosha kumwogopa na kumwonea haya Allaah ukijilinganisha wewe na Ufalme na Uadhwama Wake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
- "ما السَّماوات السّبع في الكُرسيِّ إلَّا كحلقةٍ ملقاةٍ بأرضٍ فلاةٍ ، وفضلُ العرشِ على الكُرسيِّ كفضلِ تلك الفلاةِ على تلك الحلقةِ"
“Mbingu saba kulinganisha na Kursiy si chochote isipokuwa ni kama mfano wa kijipete mviringo kilichotupwa kwenye ardhi ya jangwa kubwa, na ukubwa wa Arshi kulinganisha na Kursiy ni kama ukubwa wa jangwa hilo kulinganisha na kijipete hicho”. [Hadiyth Swahiyh Marfuw. Ibn Hibaan na Ibn Abiy Shaybah].
Sasa Allaah ‘Azza wa Jallaa Aliye Juu ya ‘Arshi hiyo Ambayo Ameielezea kama ni:
الْعَرْشِ الْكَرِيمِ
Kama Alivyosema:
"فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ"
“Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa ‘Arsh Kariym”. [Al-Muuminuwn: 116]
Na:
الْعَرْشِ الْعَظِيمِ
Kama Alivyosema:
"قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ"
“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nani Rabb wa mbingu saba, na Rabb wa ‘Arsh ‘Adhimu?” [Al-Muuminuwn: 86]….isitoshe Yeye Ndiye Aliyekuumba, Anakuruzuku, Anakupa uhai, na Anajua nyenendo zako zote, je huoni kwamba unamvunjia hishma kwa maasia yako pamoja na Uadhwama Wake huo?
Na kwa nini unajivuna kwa maasia? Jeuri hiyo unaitoa wapi? Hujui kwamba Anaweza Akakihitilafisha kiungo chochote cha mwili wako ukajikuta umepooza? Wafalme wangapi yamewakuta hayo na hata madaktari mabingwa wameshindwa kuwaponya?!
"يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ"
“Ee mwana Aadam! Nini kilichokughuri hata umkufuru Rabb wako Mkarimu”?
الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ
“Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo sura, viungo), na Akakulinganisha sawa”.
فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ
“Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza”.