20-Tukumbushane: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Uteremko Wa Allaah ‘Azza Wa Jalla Kwa Ajili Yako Kila Usiku?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

20:  Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Uteremko Wa Allaah ‘Azza Wa Jalla Kwa Ajili Yako Kila Usiku?

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"- ينزلُ اللهُ كلَّ ليلةٍ إلى السَّماءِ الدُّنْيا، حِيْنَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآخرِ، فَيَقُولُ: مَنْ يَدْعُوْنِي فأستجيبُ له ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ ، مَنْ يَسْتَغْفِرُني فأغفرُ له"

 

“Allaah Anateremka kila usiku hadi mbingu ya dunia inapobakia theluthi ya mwisho ya usiku, kisha Husema:  Nani aniombaye Nikamjibu?  Nani anitakaye haja yake Nikampa?  Nani aniombaye maghfira Nikamghufuria?”

 

Uteremko huu wa Allaah ni kwa ajili yetu Sisi kutokana na Rehma Zake.  Ni kama vile Anatufata hadi mlangoni kutuuliza haja zetu Akiwa tayari kabisa kututatulia, lakini milango yetu inabaki tumeifunga.    Hatuthamini kabisa ujio huo wa Mfalme wa wafalme!! Sisi ni nani hadi Atufanyie hivi?  Je, hii haionyeshi Penzi Lake kubwa kwetu ambalo hatulithamini wala kumthamini Mwenyewe Allaah ‘Azza wa Jalla?  Lakini je sisi tunahisi Takrima hii na Utukuzo huu Anaotupa?  Je, tunahisi thamani yake?!

 

La hasha!  Wakati huu kila mtu anakuwa amezama kwenye usingizi mkali mnono ila wachache tu waliotambua na kujua thamani ya Uteremko huu wa Allaah ‘Azza wa Jalla kwao.  Hatuoni hata aibu tukiwa gubigubi huku Yeye Anatuita ili tumuelezee matatizo yetu yaliyosheheni ya kidunia na kiaakhirah, kisha Anaondoka bila kupata jibu, lakini kwa Rahma Zake Anateremka tena usiku unaofuata kila siku na hali kubaki hivyo hivyo.  Je, hatuoni aibu?

 

Ndugu yangu!  Hii ni nafasi ya kipekee kabisa isiyo na mfano.  Pambana na usingizi wako, anza kidogo kidogo kuamka na hatimaye utazoea na kuona jambo la kawaida kabisa.  Hapo itakuwa nafasi ya kumlilia matatizo yako yote ya dunia na aakhirah, Naye bila shaka Hatokuangusha kamwe na daima Atafurahika sana nawe.

                                                             
Share