21-Tukumbushane: Kwa Nini Allaah ‘Azza Wa Jalla Anateremka Katika Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 
 

21:  Kwa Nini Allaah ‘Azza Wa Jalla Anateremka Katika Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku?

 

Allaah ‘Azza wa Jalla Ameihusisha theluthi ya mwisho ya usiku kuteremka ndanimwe, kwa kuwa huo ndio wakati wa faragha, mghafala na watu kuzama ndani ya usingizi mzito mtamu.  Ni uteremko unaolaikiana Naye Jalla Jalaaluhu ambao hakuna ajuaye namna yake ila Yeye tu.  Haufanani kabisa na wa viumbe. Na mtu kuachana na ladha ya usingizi mzito ni jambo zito sana.  Hivyo mwenye kuacha usingizi wake huo, akatawadha, akaswali na kisha akamwomba Allaah ‘Azza wa Jalla, hiyo ni dalili tosha juu ya niya yake safi, utashi wake wa kweli kwa Mola Wake, na kuwa mbali kabisa na riyaa.  Hapa Swalah yake inakuwa na khushuu halisi, duaa anaiomba kwa dhati na msisitizo huku akihisi ladha halisia ya kufanya ‘ibaadah katika wakati huu na kwa uhudhurio wa karibu kabisa wa Allaah.

 

Na kwa ajili hiyo, Allaah Huteremka kuwa karibu kabisa na watu wa aina hii. Anatuambia katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:

 

"‏إِذَا تَقَرَّبَ الْعَبْدُ إِلَىَّ شِبْرًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا، وَإِذَا تَقَرَّبَ مِنِّي ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ مِنْهُ بَاعًا، وَإِذَا أَتَانِي مَشْيًا أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً"

 

“Mja akijikurubisha Kwangu kwa shibiri, Mimi Hujikurubisha kwake kwa dhiraa, akijikurubisha Kwangu kwa dhiraa, Mimi Hujikurubisha Kwake kwa ba-‘a, na akinijia anatembea, Mimi Humjia mwendo wa haraka”.  [Swahiyh Al-Bukhaariy]

 

Shibiri au shubiri, ni kipimo cha urefu wa takriban sentimeta kati ya 20–25, ni umbali kati ya kidole gumba na cha mwisho kiganja kikitanuliwa.  Na dhiraa ni urefu wa takriban sentimeta 50, yaani kutoka ncha ya kidole cha kati hadi kwenye kisugudi.   Ama ba-’a, huo ni urefu wa mikono miwili iliyonyooshwa.  Cha muhimu, hii ni mifano tu ya vipimo, vyovyote unavyojikurubisha Kwake, Yeye inakuwa ni maradufu na ziada.

 

Na kwa vile mtu huyu amejihimu kuacha usingizi wake ili kufanya ‘ibaadah, Naye Allaah Hufurahika zaidi Naye.  Malipo yake yanakuwa kama Anavyosema Allaah:

 

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

 

Basi nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayoburudisha macho.  Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda”.  [As-Sajdah: 17]

 

Na kabla ya aayah hii, Anawasifu Akisema:

 

"تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ"

 

Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa”.  [As-Sajdah: 16]

 

Tunamwomba Allaah ‘Azza wa Jalla Atujaalie tuwe kwenye kundi hili na tuwe wawajibikaji wa kikweli.

                                         

 

Share