22-Tukumbushane: لِمَنِ المُلكُ اليَوْمَ؟ Ni Wa Nani Ufalme Wa Leo?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

22:  لِمَنِ المُلكُ اليَوْمَ؟  Ni Wa Nani Ufalme Wa Leo?

 

 

 

 

Kila siku tunasoma Suwratul Faatihah tukimsemesha Allaah na kumwambia:

 

"مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ"

 

“Mfalme wa Siku ya Malipo”.

 

Hivi kwani leo Yeye Sio Mfalme?

 

Katika maisha yetu ya hapa duniani, kila mmoja ni mfalme katika uwanja wake. Allaah Amempa kila mtu nafasi ya mamlaka maalum katika mambo fulani. Kiongozi wa nchi ana mamlaka ya kuteua anaowaona kuwa wanamfaa katika shughuli za utawala ni sawa wanafaa au hawafai.  IGP ana mamlaka ya kuteua maofisa anaowataka wa usalama, kuwahamisha hapa na pale na kadhalika, na kubeba dhamana ya usalama wa raia kiujumla.  Hata askari au mgambo tu, wakati mwingine anaingiwa na wahaka wa kutaka kuonyesha watu misuli zake, atamsimamisha mtu, amwamuru aonyeshe kitambulisho chake, akiangalie, amwamuru achuchumae, aruke kichurachura au ampe mkong’oto wakati mtu hata hana kosa lolote achilia mbali yanayojiri ndani ya mahabusu za utesaji watu ambayo ni ya kutisha na kuogofya.         Wanaotenda hayo humo wanajiona wao ni miungu watu.  Humo wao ni wafalme kwa mamlaka waliyonayo ambayo wanayatumia sivyo.

 

Hata wabeba taka za miji, ni wafalme katika kazi yao inayodharauliwa na wengi. Siku wakigoma, itabidi hata wapigiwe magoti, kwani mji unaweza usiweze kukalika kutokana na hali mbaya ya kiafya inayoweza kujitokeza.  Na hata waoshaji maiti wanaoonekana watu duni, siku wakatae kufanya kazi, itabidi kuwabembeleza na kuwalilia sana na hata ikibidi kuwaongezea malipo.  Hii ni baadhi ya mifano tu ya mamlaka aliyonayo kila mmoja kati yetu ambayo anaweza kuyatumia vibaya au kuyatumia vizuri, na hisabu yake ni Siku hiyo ya Qiyaamah. Huu ndio Ufalme wetu wa hapa duniani tuliobebeshewa dhamana na Allaah, lakini Ufalme wa Allaah pia upo.

 

Siku hiyo ya Qiyaamah utadhihirika Ufalme wa kikweli ambao watu wengi hawaujui.  Wafalme wa hapa duniani hawataonekana kabisa, kwani hawatakuwa na lolote.  Ni Ufalme wa Allaah Pekee Anayetuambia:

 

"يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ"

 

Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. Ufalme ni wa nani leo?  (Allaah Mwenyewe Atajijibu):  Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika”.   [Ghaafir: 16]

 

Yaani watu wataonekana dhahiri bayana, wakiwa uchi wa mnyama kama siku waliyozaliwa, wako pekupeku, na hawajatahiriwa au kukeketwa.  Hakuna cha kuwasitiri wala kuwaficha, si mlima, au mti, au nyumba, au pango, kwa kuwa ardhi itakuwa nyingine, si ardhi hii tunayoishi juu yake kwa sasa, bali ni ardhi nyingine kabisa isiyo na mmea, wala bahari, wala minyanyuko wala miteremko, ni ardhi iliyo mithili ya meza.  Watu kwa sasa, wanadhani kwamba wanaweza kujificha mahala fulani na Allaah ati Asiweze kuwaona wakafanya maasia.  Lakini siku hiyo wataanikwa, hakuna kwamba huyu alikuwa ni mfalme au amiri jeshi mkuu, huko utofauti utakuwa kwa amali za mtu anazozichuma hapa duniani.  Na hapa ndipo watu watakapojua ni Nani Mfalme wa kweli.  Akiuliza:  Ni wa Nani Ufalme wa leo?  Hakutokuwa na jibu.  Kimyaa, kimyaa kizito kabisa.

 

"وَخَشَعَتِ الْأَصْوَاتُ لِلرَّحْمَـٰنِ فَلَا تَسْمَعُ إِلَّا هَمْسًا"

 

Siku hiyo watamfuata mwitaji hakuna kumkengeuka.  Na sauti zitafifia kwa Ar-Rahmaan, basi hutosikia isipokuwa mchakato wa nyayo”.

 

Hapo Allaah Atajijibu Mwenyewe:  “Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika”.

Ndugu Muislamu!  Jisalimishe na siku hii ngumu kwa kuongeza matendo mema. Haya ndiyo yatakayokuweka mahala salama ukawashinda wafalme wote wa duniani ambao siku hiyo hawatokuwa na mamlaka yoyote kama haya wanayotamba nayo hapa duniani  kwa sasa.

 

                                                              

 

Share