24-Tukumbushane: Usiingie Kwenye Mkumbo Huu
Tukumbushane
24: Usiingie Kwenye Mkumbo Huu:
Ni mara nyingi tumeshuhudia sehemu mbalimbali watu wakikimbilia kupora bidhaa za lori la mizigo lililopata ajali ya kupinduka. Kupinduka huku imekuwa ni kama kihalalisho kwao kupora bidhaa hizo ambazo mwenye mali amezinunua kwa mamilioni. Nao hukusudia hasa kuvunja na kulifungua ili kupora bidhaa zilizomo humo. Na wakati mwingine inakuwa ni lori la mafuta ambayo huyafungulia ili wayachote na kuanza kumiminika kwa kiasi kikubwa na kuwa ni hatari kwao wao na kwa wengineo wasiohusika. Maafa mengi ya kutisha yametokea kutokana na tabia hii. Wenye mali wangeweza kuja, wakalinyanyua lori na kufanya mpango wa kuhamisha mali yao kwa salama kwenye gari jingine na kuifikisha kule ilikokuwa inakwenda.
Ndugu yangu Muislamu! Usijaribe kuingia kwenye mkumbo huu. Ujue kwamba ile ni mali ya mtu. Kaa mbali nayo kabisa. Kila anayepora pale, basi atakuja na mzigo huo kama ushahidi dhidi yake Siku ya Qiyaamah. Allaah Anasema:
"ومَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ"
“Na yeyote atakayekhini, atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah. Kisha kila nafsi italipwa kamilifu yale iliyoyachuma, nao hawatodhulumiwa”. [Aal ‘Imraan: 161]
Kila unayemwona pale akitoka na gunia begani au debe la mafuta, basi atakuja nalo hivyo hivyo Siku hiyo.
Halafu angalia, inakuwaje hali ya wale wanaofia hapo kwa mlipuko wa mafuta kwa mfano?! Wanakufa hali ya kuwa wanapora!! Inakuwaje hatima yao!!