25-Tukumbushane: Usiingie Kwenye Mkumbo Huu
Tukumbushane
25: Usiingie Kwenye Mkumbo Huu:
Ni mara nyingi tunashuhudia kibaka akipata kipigo kikali kisha kuchomwa moto. Kila anayepita hapo na kuona tukio, naye haraka hujiunga kupiga na kutafuta haraka zana za kuchomea mtu huyo kama tairi, mafuta, kiberiti na kadhalika bila kujua kama ni mwizi kweli au la?
Kila anayepiga, na kila anayesaidia kufanikisha zoezi la kumchoma sawa sawa kwa neno, au kwa kitendo, basi hao wote wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya nafsi mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah, na pia kesi ya kutesa na kuua kwa kutumia moto.
Kuchoma mtu au kiumbe chochote hata wadudu ni jambo lililoharamishwa. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"لا يُعَذِّبُ بالنَّارِ إلّا ربُّ النَّارِ"
“Hatesi kwa moto ila Mola wa moto”. [Hadiyth Swahiyh. Iko kwenye Al-Muhallaa (11/383)]
Na hata panya ukimkamata kwa mtego, unachotakiwa ni kumuua haraka na kwa pigo moja tu. Usimkawize baada ya kumnasa, utazidi kumtesa kisaikolojia. Muue mara moja. Mauti yanatisha hata kwa wanyama! Usimchome wala kumzamisha kwenye maji. Haya ndiyo tunayoamrishwa na Dini yetu ya kutovuka mipaka iliyowekwa na Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hali inakuwa vipi kwa mwanadamu!
Hivyo basi, ukisadifu kukutana na tukio kama hilo, jipitie zako na njia zako. Usishiriki kwa lolote, utasalimika.