26-Tukumbushane: Ukarimu Mkubwa Wa Allaah Kwa Wakosefu
Tukumbushane
26: Ukarimu Mkubwa Wa Allaah Kwa Wakosefu:
Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Anasema katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:
"قال اللهُ تعالى: يا ابنَ آدمَ! إِنَّكَ ما دَعَوْتَنِي ورَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لكَ على ما كان فيكَ ولا أُبالِي، يا ابنَ آدمَ! لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنانَ السَّماءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لكَ ولا أُبالِي، يا ابنَ آدمَ! لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الأرضِ خطَايا ثُمَّ لَقِيْتَني لاتُشْرِكْ بِيْ شَيْئًا لأتيْتُكَ بِقِرَابِها مَغْفِرَةً"
“Ee mwana wa Aadam! Hakika wewe madhali unaniomba na una matarajio mema Kwangu, basi Nitakusamehe madhambi yote uliyonayo, na wala Sijali. Ee mwana wa Aadam! Lau madhambi yako yatafikia kilele cha mbingu na pande zake zote, kisha ukaniomba msamaha, basi Nitakusamehe, na wala Sijali. Ee mwana wa Aadam! Lau utanijia na makosa yaliyojaa ardhi yote (baada ya kufa), halafu ukakutana Nami hali ya kuwa Hukunishirikisha na chochote, basi Nitakujia na maghfira ya ujazo wa makosa hayo yote”. [Hadiyth Hasan Lighayrih. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (3540) na Ahmad (13493)]
Allaah ‘Azza wa Jalla Ndiye Mwenye huruma kuliko wote wenye huruma. Yeye Ndiye Anayeghufiria na kufuta madhambi yote ya Mja Wake aliyemuasi vyovyote ukubwa wa madhambi utakavyokuwa, lakini kwa sharti ya mja huyu kuwa asiwe ni mshirikina, bali awe ni mwenye kumpwekesha Yeye tu. Washirikina hawana nafasi hii, na huu ndio ubaya wa ushirikina. Dhambi zote ziko chini ya Matakwa Yake Allaah; Anamsamehe Amtakaye, isipokuwa dhambi ya shirki. Dhambi hii Allaah Haisamehi ikiwa mtu atakufa nayo.
Katika Hadiyth hii ya Al-Qudsiy, tunaona ni namna gani Huruma ya Allaah ilivyo kubwa kwetu. Sisi wana wa Aadamu ni watu wa kuteleza sana kwenye madhambi mengi ya aina tofauti. Wengine hujisahau kabisa na kuogelea kwenye kona zote za madhambi makubwa na madogo na hata ya shirki. Lakini hawa wote, Allaah Anawasubiri wajirudi na warudi Kwake moja kwa moja ili Apate kuwasamehe na kuwafutia makosa yao yote bila Yeye kujali ukubwa wa makosa yao hayo, na hata bila ya kuwawekea masharti ya aina yoyote. Muhimu warejee Kwake kidhati na wawe tayari. Anatuambia:
"قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ"
“Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu”. [Az-Zumar: 53]
Mbali na wito huu mwema wa kutubembeleza pamoja na madhambi yetu na kwamba tusikate kabisa tamaa na Rahmah Zake, na kwamba Yeye Anasamehe madhambi yote, Anaendelea kutuambia:
"وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ"
“Na rudini kwa Rabb wenu (kwa tawbah na matendo mema), na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu, kisha hamtonusuriwa”.
Na haya ni hapa duniani kabla ya mtu kufariki. Kama atafariki na madhambi, Allaah pia huko Aakhirah Atamsamehe madhambi yake kama hana dhambi ya shirki. Ndio hapo Anapotuambia:
"يا ابنَ آدمَ إنَّكَ لو أتيتَني بقرابِ الأرضِ خطايا ثمَّ لقيتَني لا تشرِكُ بي شيئًا لأتيتُكَ بقرابِها مغفرةً"
Ee mwana wa Aadam! Lau hata utanijia na makosa yaliyojaa ardhi yote (baada ya kufa), halafu ukakutana Nami hali ya kuwa Hukunishirikisha na chochote, basi Nitakujia na maghfirah ya ujazo wa makosa hayo yote.
Ulamaa wanasema madhambi makubwa aliyoyafanya Muumini yanahitajia kuomba tawbah, au suala la kusamehewa liko katika Mikono ya Allaah; Akitaka Atamsamehe, na Akitaka Atamwadhibu. Kadhalika, haki za watu ni lazima zirejeshwe, au Allaah Anaweza kumlipa mwenye haki kwa Fadhla Zake na kumsamehe kwa Ukarimu Wake aliyedhulumu.
Tunajifunza kutokana na Al-Hadiyth Al-Qudsiy hii:
1- Fadhla ya tawhiyd. Tawhiyd ndio sababu pekee ya Muumini kuepukana na adhabu za Allaah.
2- Shirki ni hatari mno, inabidi iepukwe kwa njia zote.
3- Ukarimu mkubwa usio na mipaka wa Allaah kwetu. Vyovyote madhambi yetu yatakavyokuwa makubwa hadi kujaza mbingu zote, Allaah Huyasamehe mja akirudi Kwake na kumwomba maghfirah.
4- Umuhimu wa kuomba duaa na kuomba maghfirah.
5- Umuhimu wa kuwa na rajua njema kwa Allaah.
6- Uharamu wa kukata tamaa na Rahma za Allaah.