27-Tukumbushane: Siri Kubwa Ya Kumsabbih Allaah

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

27:  Siri Kubwa Ya Kumsabbih Allaah:

 

Ukifuatilia suala la Allaah kusabihiwa kwenye Qur-aan Tukufu, utakuta ajabu kubwa.

 

1-  Utakuta kwamba “Tasbiyh” ina uwezo wa kuondosha Qadari ya Allaah.  Katika kisa cha Nabiy Yuwnus ‘Alayhis Salaam, Allaah Anatuambia:

 

"فَلَوْلَا أَنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُسَبِّحِينَ  • لَلَبِثَ فِي بَطْنِهِ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ"

 

Na lau kama hakuwa miongoni mwa wenye kumsabbih Allaah •  Angelibakia tumboni mwake mpaka Siku watakayofufuliwa”.  [Yuwnus: 143-144].

 

Alikuwa anasema katika kumsabbih Allaah:

 

"لا إِلَهَ إِلاّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّيْ كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِيْنَ"

 

2-  Utakuta kwamba “tasbiyh” ndiyo utajo ambao milima na ndege ilikuwa ikiitikia pamoja na Nabiy Daawuwd ‘Alayhis Salaam.  Allaah Anatuambia:

 

"وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ"

 

“Na Tukatiisha milima iwe pamoja na Daawuwd ikisabihi pamoja na ndege”.   [Al-Anbiyaa: 70]

 

3-  “Tasbiyh” ni utajo wa viumbe vyote ulimwenguni; mbinguni na ardhini.  Allaah Anatuambia:

 

"أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ ۖ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ"

 

“Je, huoni kwamba wanamsabihi Allaah walioko mbinguni na ardhini, na (pia) ndege wakiwa wamekunjua mbawa zao.  Kila mmoja (Allaah) Amekwishajua Swalaah yake na tasbihi yake.  Na Allaah Ni Mjuzi kwa yale wayafanyao”.  [An-Nuwr: 41]

 

4-  Zakariyyaa ‘Alayhis Salaam alipotoka mihrabuni kwake, aliwaamuru watu wake walete “Tasbiyh”.  Allaah Anatuambia:

 

"فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ أَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا"

 

Basi akawatokea watu wake kutoka mihrabuni, akawaashiria: Msabihini (Allaah) asubuhi na jioni”.  [Maryam: 11]

 

5-  Nabiy Muwsaa ‘Alayhis Salaam alimwomba Allaah Amfanye nduguye Haaruwn kuwa msaidizi wake atakayemsaidia katika kumsabbih Allaah na kumtaja.  Anatuambia Allaah:

 

"وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي هَارُونَ أَخِياشْدُدْ بِهِ أَزْرِي  وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًاوَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا"

 

Na Nifanyie msaidizi kutoka ahli zangu •  Haaruwn, ndugu yangu Nitie nguvu kwaye Ili tukusabihi kwa wingi •  Na tukudhukuru kwa wingi”.  [Twaahaa: 29-34]

 

6-  “Tasbiyh” ndiyo utajo wa watu wa Peponi.  Allaah Anatuambia:

 

"دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ"

 

Wito wao humo ni: Utakasifu ni Wako ee Allaah.  Na maamkizi yao humo ni Salaamun!”  [Yuwnus: 10]

 

7-  “Tasbiyh” ni utajo wa Malaika.  Allaah Anatuambia:

 

"وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ"

 

“Na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini”.  [Ash-Shuwraa: 05]

 

8-  “Tasbiyh” imekuja kwa vitenzi tofauti katika Qur-aan.

 

(a)  Cha wakati uliopita.  Allaah Anasema:

 

"سَبَّحَ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ"

 

“Vimemsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote”.  [Al-Hadiyd: 01].

 

(b)  Cha wakati uliopo.  Anatuambia Allaah Ta’aalaa:

 

"يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ"

 

Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote”.  [Al-Jum-‘ah: 01]

 

(c)  Kitenzi agizi.  Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى"

 

“Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Aliyetukuka kabisa kuliko vyote”.  [Al-A’alaa: 01]

 

Vitenzi vyote hivi viko katika Aayaati za mwanzo za Suwrah.  Na hapa bila shaka kuna siri kubwa.

 

9-  “Tasbiyh” ni sababu ya kupata mambo ya kumridhisha na kumfurahisha Muislamu duniani na aakhirah.  Allaah Anatuambia:

 

"فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ"

 

Basi subiri juu ya yale wanayoyasema.  Na sabihi ukimhimidi Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla ya kuchwa kwake.  Na katika nyakati za usiku pia sabbih na katikati ya mchana, lazima utapata ya kukuridhisha”.  [Twaahaa: 130]

 

Na ili kuyapata hayo, Allaah Anatuhimiza hapa tumsabbih nyakati hizi tajwa na nyakati zingine zote.

 

10-  “Tasbiyh” ni ponyo la dhiki ya kifua na kisaikolojia.  Allaah Anasema:

 

"وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ"

 

Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema • Basi sabihi na mhimidi Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu”.  [Al-Hijri: 97-98]

 

 

Angalia namna Aaayah hii inavyoelekeza namna ya kuondosha dhiki ya kifua na roho kwa ‘Tasbiyh”.  Ukihisi hali hiyo, basi kimbilia kumsabbih Allaah, ni dawa ya ponyo.

 

Haya yote yanaonyesha siri kubwa iliyoko ndani ya “Tasbiyh”.  Ulimwengu wote wa juu na wa chini, av yote vilivyomo humo vinamsabbih Allaah; kila kimoja kwa namna yake Anayoijua Allaah.  Muislamu usije ukajitoa ndani ya duara hilo. Usije kuwa ndani ya kundi la walioghafilika.  Ni amali rahisi kabisa ya ulimi isiyohitajia zana, wala wakati maalum wala sehemu maalum.  Usipoteze nafasi hii muhimu.

 

Kati ya “Tasbiyh” bora kabisa na zenye malipo makubwa ni:

 

سُبْحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِه عَدَدَ خَلْقِهِ وَرِضَا نَفْسِهِ وَزِنَةَ عَرْشِهِ وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ

 

                                                                        

Share