28-Tukumbushane: Tuambulie Angalau Yai Zima

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

28:  Tuambulie Angalau Yai Zima:

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمْعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ، ثُمَّ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الأُوْلَى فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الرَّابِعَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ دَجَاجَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الْخَامِسَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَيْضَةً، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ حَضَرَتِ الْمَلاَئِكَةُ يَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ ‏"

 

“Mwenye kuoga kikamilifu siku ya Ijumaa kama anavyofanya katika ghuslu ya janaba, kisha akaenda (Msikitini) katika saa la mwanzo, basi anakuwa kama ametoa swadaqah ngamia, na mwenye kwenda saa la pili, anakuwa kama ametoa swadaqah ng’ombe, na mwenye kwenda saa la tatu, anakuwa kama ametoa swadaqah kondoo dume mwenye pembe, na mwenye kwenda saa la nne, anakuwa kama ametoa swadaqah kuku, na mwenye kwenda saa la tano, anakuwa kama ametoa swadaqah yai.  Na Imamu anapotokeza (akapanda mimbari), Malaika huingia na kuketi kusikiliza utajo”.   [Hadiyth Swahiyh.   Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)]

 

Allaah Ta’aalaa Ametuamuru tuharakie kwenye mambo yote ya kheri. Anatuambia:

 

"فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِين"

 

Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake. Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya khayr na wakituomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea.  [Al-Anbiyaa: 90]

 

Kwenda mapema kwenye Swalah ni katika jambo muhimu sana la kheri na hususan Swalah ya Ijumaa kwa wanaume.  Katika Hadiyth hii, Rasuli anatueleza thawabu zinazopatikana kwa mujibu wa saa kwa saa.  Anayekwenda Msikitini Siku hii ya Ijumaa katika saa la mwanzo, basi thawabu zake ni sawa na aliyetoa ngamia swadaqah, na la pili sawa na ng’ombe, la tatu sawa na kondoo, la nne sawa na kuku, na la tano na la mwisho sawa na yai.

 

Masaa Haya Matano Hugawanywaje Au Hupatikanaje?

 

Masaa haya huanza kuhesabiwa kuanzia pale jua linapochomoza mpaka adhana ya pili ya Ijumaa.  Kwa mfano, kama jua linachomoza saa 06.30 a.m (kumi na mbili na nusu asubuhi), na adhana ya pili ya Ijumaa ni saa 12.30 p.m (sita na nusu mchana), hapa kutakuwa na jumla ya masaa sita yenye dakika 360 (60X6).  Lakini sisi tunataka masaa matano tu kama yalivyoainishwa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Ili kuyapata, tutagawa dakika hizo 360 kwa tano (ambayo ni masaa tajwa katika Hadiyth (360÷5) na tutapata dakika 72 kwa kila saa moja.  Hivyo basi, jedwali ya masaa na thawabu ya vilivyotajwa itakuwa kama ifuatavyo:

 

 

Masaa

Kuanzia - Hadi

Thawabu

 

 

 

La Kwanza

6.30 a.m hadi 7.42 a.m

Saa 12 na nusu asubuhi hadi saa moja na dakika 42.

 

Ngamia

 

La Pili

7.42 a.m hadi 8.54 a.m

Saa moja na dakika 42 hadi saa mbili na dakika 54.

 

Ng’ombe

 

La Tatu

8.54 a.m hadi 10.06 a.m

Saa mbili na dakika 54 hadi saa nne na dakika sita.

 

Mbuzi, kondoo

 

La Nne

10.06 a.m hadi 11.18 a.m

Saa nne na dakika sita hadi saa tano na dakika 18.

 

Kuku

 

La Tano

11.18 a.m hadi 12.30 a.m

Saa tano na dakika kumi na nane hadi saa sita na nusu.

 

Yai

 

 

Thawabu hizi pia hutofautiana ndani ya kila saa kwa mujibu wa mtu atakavyowahi.  Ikiwa kwa mfano saa la kwanza ngamia wake ni wa uzito wa kilo 1000, basi anayeingia Msikitini dakika ya mwanzo kabisa ya saa kumi na mbili na nusu, basi huyo atampata huyo wa kilo 1000.  Na huyu pia atasajiliwa nambari moja na Malaika wanaosimama kwenye milango ya Msikiti kuwasajili wote wanaoingia kwa ajili ya Swalah katika siku hiyo.  Ni mafanikio yalioje ya kusajiliwa nambari moja!   Mwingine kwa uvivu wake na mapuuza, hata nambari ya mwisho haipati.  Ni wale wanaotegea hadi khatibu apande mimbari, kisha wajikongoje wafike mwisho wa khutba ya pili.  Hapa Malaika wanakuwa wameshafunga madaftari yao zamani na kuingia Msikitini kusikiliza utajo wa Allaah kwenye khutbah.  Ni hasara kubwa sana kwa Muislamu, kwa hakika. Anayekuja baada ya robo saa 6.45 am, basi atapata wa kilo 750 na kuendelea.  Hali kadhalika katika masaa mengineyo hadi kwenye yai.  Mwingine atapata la ukubwa wa mbuni, mwingine mpaka wa ndege mdogo kabisa.  Je, hata hili pia litamshinda Muislamu kulipata kwa hao wanaotegea kuja saa la mwisho kabisa!

 

Huenda mtu akadharau kuona kwamba thawabu za yai ati ni ndogo mno!   Hajui zina thamani gani mbele ya Allaah Anayezitoa.  Hamfikirii pia anayepata ngamia, ni namna gani anasubiri huyu!  Kukaa ndani ya Msikiti kwa masaa sita na hadi kumalizika khutba na Swalah, si jambo dogo hata kidogo, na huenda hakuna anayeweza kufanya hilo kwa sasa isipokuwa wachache mno, au hata wasipatikane kabisa.  Wanaopatikana huenda ni wa ng’ombe kuanzia saa lake la mwisho.  Tujitahidini ndugu Waislamu tupate angalau kuanzia kondoo, na tukishindwa sana, hata yai kamili.

 

Pamoja na hayo yote, thawabu zilizotajwa ni mfano tu, lakini kiuhakika ni thawabu kubwa zaidi na zaidi hata za hilo yai. Ndio maana Rasuli akasema “ni kama”.  Na mwenye kuchelewa akazikosa thawabu hizo, hakosi pia fadhila za Siku hii tukufu.  Hizi ni katika Fadhila za Allaah kwetu.  Na katika kukamilisha malipo hayo, Muislamu asisahau kuoga vizuri mwogo maalum kwa ajili ya Siku hiyo ili kupata malipo kamili kabisa.  Atumie shampoo kuosha nywele za kichwa, asugue mwili na hususan kwato mbili, baadhi hujisahau hadi kwato kutoa mipasuko, akate nywele za kinena, za kwapa na kadhalika ili kufanya malipo yawe kamili, halafu avae nguo nzuri na ajitie manukato.

                                                   

 

 

Share