29-Tukumbushane: Lituzindushe Hili

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

29:  Lituzindushe Hili:

 

Tumesikia na kushuhudia tukio la kutokea tetemeko kubwa nchini Uturuki na Syria tarehe 05/02/2023.  Maelfu ya watu walikufa, maelfu wengine walijeruhiwa, na maelfu wengine walioponea walipoteza kila kitu kuanzia nyumba zao na vyote vilivyomo ndani, mbali na maelfu pia waliowapoteza ndugu zao, jamaa zao na kadhalika.  Bila shaka ni mtihani na msiba wa kushtua sana. Unahitaji subra ya hali ya juu kabisa kuukabili.

 

Tetemeko kwa kweli linatisha na kuogofya sana.  Wale waliolikabili wakiwa ndani ya majengo na hasa marefu, hao ndio kiukweli wanajua maana halisi ya tetemeko. Utakuta jumba lote linayumba pamoja na uzito wake wote, sauti kali ya vyote vilivyomo ndani ya nyumba vikigongana na kucheza huku na kule pamoja na mtikisiko wa ajabu.  Tetemeko hili la Uturuki na Syria, ukubwa wake ni wa nyuzi 7 na nukta kadhaa hivi kwa kipimo cha Rechter, na athari zake ndizo hizo kama zinavyoonekana kwenye vyombo vya habari.   Sasa hilo la Qiyaamah litakuwaje?

Allaah Anatuambia:

 

"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ •  َوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ"

 

“Enyi watu!  Mcheni Rabb wenu, hakika zilizala la Saa (Qiyaamah) ni jambo kuu •  Siku mtakapoiona, kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu wamelewa, kumbe hawakulewa lakini ni Adhabu ya Allaah kali”.  [Al-Hajj: 01-02] 

 

Tukio kama hili linapotokea, hakuna mtu anashughulika na mwingine. Analoangalia wakati huo ni kujiokoa mwenyewe kwanza.  Katika Hadiyth iliyohadithiwa na Mama yetu ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلاً ‏.‏ قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، النِّسَاءُ وَالرِّجَالُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟ قَالَ صلى الله عليه وسلم: ‏"‏يَا عَائِشَةُ، الأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ‏"‏ ‏.‏

 

“Watu watakusanywa Siku ya Qiyaamah wakiwa miguu peku peku, uchi wa mnyama bila nguo, hawajatahiriwa”..  Bibi ‘Aaishah alishtuka na kusema:

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Na wanawake na wanaume wote watatazamana (nyuchi)! Rasuli akamwambia:  Ee ‘Aaishah!  Mambo yatakuwa ni magumu mno kuweza hata kuangaliana”.   [Swahiyh Al-Bukhaariy (6527)]

 

Hawatoweza kuangaliana kutokana na kizaa zaa cha Siku hiyo, kila mtu roho juu juu akiifikiria nafsi yake tu, hata Mitume pia, isipokuwa Muhammad (Swalla Allaah ‘alyhi wa aalihi wa sallam) ambaye atakuwa anauombea umati wake badala ya nafsi yake.  Tutafufuliwa bila kitu chochote, vyote tulivyokuwa navyo hapa duniani, tutakuwa tuliviacha tulipoiaga dunia, na tutarudi tena kwa Allaah kama ile siku ya mwanzo Alipotuumba.

 

"كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ"

 

“Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena.  Ni ahadi iliyo juu Yetu. Hakika Sisi Ni Wenye Kufanya”.  [Al-Anbiyaa: 104]

 

Tukio hili ni nafasi kwetu ya kuwa tunakumbushwa.  Ndugu zetu waliofariki walikuwa ndani ya majumba yao wakiwa katika hali ya usalama na amani.  Lakini nyumba hizo hizo zikageuka ghafla na kuwa zana ya kuwatoa uhai wao.  Ghafla bila kutarajia wamejikuta washahamia kwenye maisha mengine ya barzakh kusubiri baragumu la pili la Qiyaamah.  Wengi wetu tunakiona Qiyaamah kama vile kiko mbali sana.  La hasha!  Kiko karibu sana kuliko tunavyodhania.  Mtu unapokufa, basi Qiyaamah chako kidogo kishasimama, kwa maana unakuwa umeshaingia katika duara la kwanza la Qiyaamah la maisha ya kaburini ukisubiri duara la pili la Qiyaamah kikuu cha kufufuliwa na kutoka makaburini, na kisha yanayofuatia baada ya hapo.  Tujiandae vyema kwa hayo yote.

                                        

 

Share