30-Tukumbushane: Zoezi La Kila Siku

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

30:  Zoezi La Kila Siku:

 

Kila siku tunalala na kuamka.  Kabla ya kulala, tunatayarisha vizuri kitanda kwa ajili ya kupata usingizi mzuri.  Baada ya kupanda kitandani, huwa tunajaribu kuutafuta usingizi.  Usingizi huu kama ujulikanavyo ni mauti madogo.  Na mauti haya madogo, yaani usingizi wenyewe, hauji ila baada ya roho kutoka mwilini. Unastukia tu usingizi umekuchukua bila kujua umekujaje.  Hapo roho inakuwa imetoka mwilini, kwani usingizi hauji ila kwa kutoka roho mwilini.  Yeyote umwonaye kalala, basi ujue roho yake haipo, hapo anakuwa ndani akossa madogo.  Viungo vyake vyote vya nje vinakuwa vimetulia tuli, na kinachobakia kikifanya kazi ni masikio tu.   Allaah Anatuambia:

 

"اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ"

 

“Allaah Huzichukua roho wakati wa kufa kwake, na zile zisizokufa katika usingizi wake, kisha Huzizuia ambazo Amezikidhia mauti, na Huzirudisha nyingine mpaka muda maalumu uliokadiriwa.  Hakika katika hayo bila shaka kuna ishara kwa watu wanaotafakari”.   [Az-Zumar: 42]

 

Ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anaamka husema akimshukuru Allaah:

 

"الحَمْدُ لله الذِيْ أَحْيَانَا بَعْدَ مَا أَمَاتَنَا وَإِلَيْهِ النُّشُوْرُ"

 

“Himdi ni Yake Allaah Ambaye Ametuhuisha (Ametuamsha) baada ya Kutufisha (Kutupa usingizi), na Kwake ndio ufufuo”.  [Al-Bukhaariy (6324)]

 

Hivyo basi, usingizi wetu huu ni kama zoezi la kila siku la kuandaliwa akossa makubwa ya roho kutoka na kutorejea tena mwilini.  Mauti hayo ni tofauti na haya madogo.  Hayo yana sakaraat, yana vishindo, yana kufunuliwa pazia la kumwona Malaika wa kutwaa roho (Malakul Mawt) na Malaika wengineo wa adhabu au wa rahmah, na mengi mengineyo yanayohusiana na zoezi hilo na yanayofuatia.  Hapo tutaona yote tunayohadithiwa na Qur-aan kwa mujibu wa hali ya mtu.  Allaah Anatuambia:

 

"لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ"

 

“(Aambiwe): Kwa yakini ulikuwa katika mghafala na haya!  Basi Tumekuondoshea kifuniko chako, basi kuona kwako leo ni kukali”.   [Qaaf: 22].

 

Ndugu Muislamu!  Kama unavyotandika kitanda chako kwa shuka nzuri, mito mizuri na mablanketi mazuri ili upate usingizi mnono, basi ujue kitanda hiki pia ni kama kaburi lako dogo la mauti madogo.  Na kama unavyokitayarisha hivyo, basi litayarishe pia kaburi lako kubwa baada akossa makubwa kwa kila amali njema, na kujiepusha na kila baya, madhambi, dhulma na akossa mengineyo. Hilo haliepukiki, na safari yake ni ndefu.

 

 

 

Share