31-Tukumbushane: Tuwe Tayari Kwa Majibu

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

31:  Tuwe Tayari Kwa Majibu:

 

Kila kitu kinachotoka kwenye mwili wa mwanadamu kinaonekana ni kichafu kuanzia haja ndogo na kubwa, jasho la mwili, kamasi, kohozi, mate na hata manii ambayo ndio tumeumbwa nayo.  Kila kimoja kati ya hivi kinatofautiana na kingine kwa mujibu wa kilivyo.  Na hata matapishi ambayo ni chakula kizuri kilichoingia tumboni na kuanza kuchakatwa, kama yatatoka mtu akatapika, basi watu kuyaangalia mara mbili inakuwa ni mtihani.  Matapishi haya ndiyo huja kufyonzwa na mwili na kupelekwa maeneo tofauti ikiwemo sehemu ya kutengenezewa maji ya uzazi ambayo hatimaye hutulia katika sehemu yake kusubiri yachupishwe na kutulia kwenye ukuta wa tumbo la uzazi na kuanza mchakato baada ya mchakato hadi mtu kuzaliwa.  Wote tumepitia mchakato huo, hakuna wa kubisha.  Na hata manii hayo pia yanaonekana ni kitu kichafu ingawa si najisi.

 

Mada hizi zinazotoka mwilini kama hazikuangaliwa kwa usafi stahiki, basi mtu atakuwa hakaribiki kutokana na harufu.  Mtu akivaa soksi kwa siku mbili mfululizo bila kubadili, bila shaka ataudhi watu sana kwa harufu kali ya miguu. Mtu akilala, hata akapiga mswaki kabla ya kulala, akiamka atakuta kinywa kimekwishataghayuri kwa harufu.  Nguo nazo inabidi kubadili takriban kila siku, la sivyo mambo yataharibika.

 

Hali hii ya maumbile yetu, huenda Allaah Ametuumbia nayo ili tujitathmini na kuondosha sifa ya kiburi.  Ni kama tunaambiwa kuwa ukiwa hai hali yako ni hii, sasa ukifa, basi mambo yatakuwaje!  Na kwa ajili hiyo, mtu akifa tunaamuriwa tumzike haraka iwezekanavyo kabla hajaanza kuharibika.  Hapa hakuna tofauti kati ya tajiri wala masikini, wala kiongozi wala raia, wote ni hali moja.

 

Huenda pia hali hii ikatufanya tupate ladha halisi ya Pepo, kwa kuwa Peponi hakuna hali kama hizo.  Mtu mwenye njaa kali, ndiye anayehisi ladha halisi ya chakula hata kwa kipande cha mkate mkavu, kama huna njaa, basi hata chakula kiwe kizuri vipi, hutoweza kuburudika nacho itakikanavyo.

 

Kadhalika, inawezekana kuwa Allaah Anatutakia kheri zaidi kutokana na maumbile haya.  Anataka tupate thawabu zaidi wakati tukijitahidi kwa usafi ili tusiwaudhi watu kwa harufu za kinywa, harufu ya kikwapa na harufu nyinginezo.  Muislamu hulipwa thawabu kwa juhudi kama hizi za usafi, na ni jambo ambalo Allaah pia Hulipenda kama Anavyosema:

 

"إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ"  

 

“Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia mara kwa mara, na Anapenda wenye kujitwaharisha”.  [Al-Baqarah: 222]

 

Kiufupi, huenda hali hii ya vinavyotoka mwilini inatukumbusha pia kwamba sisi ndio tuliokirimiwa zaidi kuliko viumbe wengine kwa upande wa vyakula, mbogamboga, matunda na vinywaji ambayo imepelekea maumbile yetu yawe hivi.  Hebu jaribu kuhesabu aina za vyakula, aina za mbogamboga, aina za matunda, aina za vinywaji nk.  Hesabu aina za mafuta ya kupikia, samli za aina tofauti na vinginevyo vingi.  Hivi vyote tunavila na kuvinywa na kuingia ndani ya miili yetu.  Ni neema kubwa kwa kweli.  Wanyama wala nyama ni nyama tu basi, hawahitaji tunda wala chai, ndege walao nafaka au wadudu, ni hivyo tu walavyo basi, hawahitajii juisi wala kahawa.  Lakini sisi na hasa wenye uwezo, vinavyoliwa havihesabiki.  Na haya yote tutakwenda kuulizwa ni vipi tuliyatumia.  Hakuna neema ya bure tu hivi.

 

"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ"

 

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema”.  [At-Takaathur: 08]

Tujiandae na majibu katika Siku hiyo ngumu kabisa.

                                                          

 

 

Share