32-Tukumbushane: Ni Muda Mfupi Sana
Tukumbushane
32: Ni Muda Mfupi Sana:
Mtu akilala na kuamka, ukamuuliza hapo hapo ni saa ngapi, bila shaka hawezi kukujibu. Ili kukujibu, ataitafuta saa. Ukimuuliza ni masaa mangapi kalala, pia hawezi kuwa na jibu.
Na mtu aliyepoteza fahamu pia, kwa ajali au kwa sababu nyingine yoyote, akirudisha fahamu, basi hawezi kujua muda aliopoteza fahamu mpaka aambiwe na yote yaliyojiri.
Vijana waliokimbilia pangoni, Allaah Aliwalaza kwa muda wa miaka 309. Lakini Alipowaamsha, walihisi kama wamelala kwa muda wa siku moja tu au sehemu ya siku. Hawakujua kabisa kama wamelala muda wote huo wa karne tatu. Haya yote ni kwa kuwa wakati mtu anapolala, anakuwa hana tena mahusiano na wakati. Kwa kuwa tunapokuwa macho, wakati tunauhisi kwa kufuatilia mwenendo wa jua, au kwa kutizama saa na kadhalika. Mtu kama hana saa, wala halioni jua, hawezi kabisa kujua wakati. Ni kama watu waliofungwa jela ndani ya jela.
Na wakati tutakapokufa, tutaingia katika kanuni nyingine kabisa tofauti na kanuni za maisha yetu ya dunia. Huko hakuna jua la kutujulisha wakati, au mwezi wa kutujulisha miezi au miaka. Angalia -kama inavyotueleza Qur-aan- mfano wa mtu yule aliyepita kwenye kijiji, akakikuta kimeporomoka na kubaki magofu tu. Akajiuliza vipi Allaah Ataweza kukirejesha tena kama kilivyokuwa pamoja na watu wake waliokuwa wakiishi ndani yake?! Allaah Akamfisha mtu yule kwa muda wa miaka 100. Alipomfufua, Akamuuliza -kupitia kwa Malaika Wake- muda aliokaa pale akiwa maiti. Akajibu ni siku moja au baadhi ya siku. Ni sawasawa na walivyohisi vijana wa pangoni. Allaah Akamwambia kwamba amekaa pale kwa muda wa miaka 100, na chakula chake hakikuharibika wala kinywaji chake, lakini punda wake tu aliyekufa ndiye aliyebakia mifupa. Haya yote yanaelezwa na Aayah ya 259 ya Suwrat Al-Baqarah kuonyesha Uwezo wa Allaah.
Wengi wetu tunakiona Qiyaamah kama kiko mbali sana, na kwamba kwenye makaburi tutakaa sana kukisubiri. La hasha! Kiko karibu kuliko tunavyodhania. Tutakapokufa, basi hapo kaburini kwenye maisha ya barzakh, ndio tutakuwa kwenye kituo cha kwanza cha aakhirah. Hapo hakuna saa ya kujua wakati, au jua la kuzama na kuchwa la kutujulisha siku mpya, au mwezi wa kutujulisha mwezi mpya wa hijria, huko mambo ni mengine kabisa. Watu watakuwa wanapambana na adhabu za kaburi, au wananeemeka na neema zake, huko pengine kuna nyakati za kihuko tofauti na za kidunia. Tahamaki, watashitukia baragumu la pili linapulizwa na wanatoka makaburini kukabiliana na mengineyo yanayofuatia baada ya kufufuliwa. Rabbi tunaomba Hifadhi Yako Siku hiyo ngumu kabisa. Tunaomba tuwe salama kwenye Kivuli Chako. Tunaomba Tusalimike na kitisho na kizaazaa kikubwa cha Siku hiyo.
Hapo waliokaa makaburini miaka mamilioni, na waliokaa kwa wiki, wote watajiona kama wamekaa huko siku moja au sehemu ya siku tu. Qaabiyl na Haabiyl wakifufuliwa leo, basi watajiona kama wamekaa makaburini kwao siku moja tu au sehemu ya siku.
"كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَهَا لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا عَشِيَّةً أَوْ ضُحَاهَا"
“Siku watakapoiona, watakuwa kama kwamba hawakubaki (duniani au makaburini) isipokuwa jioni moja au mchana wake”. [An-Naazi’aat: 46]
Na hapa ndipo tutakuja kugundua kwamba si umri wa ulimwengu, wala umri wa dunia yetu, wala umri wa maisha yetu ya duniani na ya barzakh, isipokuwa ni muda mfupi na mchache sana.