33-Tukumbushane: Neema Ya Chakula

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

33:  Neema Ya Chakula:

 

Kila siku tunakula na kunywa. Tukitaamuli safari ya chakula tulichotengewa mezani au mkekani, tutakuta safari yake ni ndefu kuanzia kilipokuwa mbegu shambani, kukua hadi kukomaa, kuvunwa na kufikishwa sokoni hadi mezani mbele yako.   Hii ni katika neema kubwa za Allaah ambazo wengi tunaghafilika nayo.   Allaah Akituzindusha kuhusu neema hii Anatuambia:

 

 

"فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ •  أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا • ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا • فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا • وَعِنَبًا وَقَضْبًا • وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا • وَحَدَائِقَ غُلْبًا • وَفَاكِهَةً وَأَبًّا • مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ"

 

Basi atazame mwana Aadam chakula chake • Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu • Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea) • Tukaotesha humo nafaka • Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena) • Na mizaituni na mitende • Na mabustani yaliyositawi na kusongamana • Na matunda na majani ya malisho ya wanyama • Yakiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo”.   [‘Abasa: 24-32].

 

Kila neema tuliyopewa na Allaah, basi tujue ina thamani yake, na thamani yake ni kuitunza vyema, kuitumia vyema na kumshukuru Allaah.  Kila neema tuliyonayo, iwe ndogo, iwe kubwa, basi kwa hakika, bila shaka, tutakuja kuulizwa Siku ya Qiyaamah.   Allaah Anatuambia:

 

"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ "

 

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema.  [At-Takaathur: 08]

 

Miongoni mwa vipengele vya kushukuru neema ya chakula au kinywaji, ni kumhimidi Allaah baada ya kumaliza kula.  Matamshi mengi ya himdi na du’aa yamethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kula.   Kati yake ni:

 

1-  "الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي كَفَانَا وَأَرْوَانَا، غَيْرَ مَكْفِيٍّ، وَلاَ مَكْفُورٍ" 

 

“Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Ametutosheleza mahitajio yetu na Akatuondoshea kiu, hazilipiki (Fadhila Zake) wala hazikanushiki”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5459)].

 

2- "الْحَمْـدُ للهِ حَمْـداً كَثـيراً طَيِّـباً مُبـارَكاً فِيْهِ، غَيْرَ مَكْفِيٍّ وَلا مُوَدَّعٍ وَلا مُسْتَغْـنىً عَنْـهُ رَبَّـنا"

 

“Himdi Anastahiki Allaah, himdi zilizo nyingi, zilizo njema na zilizojaa baraka tele ndani yake, haziwezi kulipika, wala kuachwa, wala kutohitajiwa tena, ee Rabbi wetu”.   [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5458), Abu Daawuwd (3849), Ibn Maajah (3284 na Ahmad (5/256)].

 

3- "الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِيْ أَطْعَمَ وَسَقَى وَسَوَّغَهُ وَجَعَلَ لَهُ مَخْرَجًا"

 

“Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Amelisha, Amenywesha, Akakifanya (chakula) kuwa chepesi kuingia mwilini, na Akakiwekea njia ya kutoka mwilini.”   [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3851) na Ibn As-Sunniy].

 

4- "اللّهُمَّ أَطْعَمْتَ وَسَقَيْتَ وَأَغْنَيْتَ وَأَقْنَيْتَ وَهَدَيْتَ وَأَحْيَيْتَ، فَلَكَ الحَمْدُ عَلَى مَا أَعْطَيْتَ"

 

“Ee Allaah!  Umelisha, Umenywesha, Umetosheleza, Umekinaisha, Umeongoa, na Umehuisha.  Basi ni Yako Himdi kwa yote Uliyotoa”.   [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad katika “Al-Musnad” nambari 1600].

 

Duaa hizi ni sehemu ya kutusaidia maswali yanayotusubiri Siku hiyo.

 

 

 

Share