34-Tukumbushane: Vinywaji Ni Katika Neema Kubwa Kwetu

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

34:  Vinywaji Ni Katika Neema Kubwa Kwetu:

 

Tukijaribu kuhesabu vinywaji vya halali tunavyotumia, bila shaka tutakuta ni vingi sana kuanzia vya moto hadi vya baridi.   Tuna chai ambayo inajulikana na watu wote na imekuwa ni katika biashara kubwa zinazoongoza duniani ikifuatiwa na kahawa.  Tuna maziwa, vinywaji baridi vya aina mbalimbali, juisi na kadhalika bila kusahau maji ambayo yanawashirikisha viumbe wote hai.

 

Vinywaji vyote hivi tunavyovitumia, ni katika neema kubwa kabisa tulizokirimiwa na Allaah Ta’aalaa kama wanadamu kulinganisha na viumbe wengine.   Na kwa ajili hiyo, tunatakikana tuitumie neema hii kwa njia inayomridhisha Allaah kwa kutokufanya israfu au mengine yasiyostahiki kama Anavyotuambia:

 

"وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ"

 

“Na kuleni na kunyweni, na wala msifanye israfu, hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu”.   [Al-A’araaf: 31]

 

Israfu ni tabia mbaya inayomchukiza Allaah.  Tabia hii inahatarisha mtu kunyan’ganywa neema yoyote aliyopewa na Allaah Mtukufu.  Israfu ni kutumia kitu katika halali lakini kwa ziada isiyohitajika.  Mfano mdogo tu ni yale yanayoshuhudiwa kwenye mialiko ya walima na mingineyo ambapo sinia ya kuliwa na watu sita, wanawekewa watu wawili tu, na kinachobaki kinamwagwa. Tabia hii kwa kiasi kikubwa imepungua sana pengine kutokana na gharama za maisha kupanda, au watu kiasi fulani kujirekebisha na tabia hiyo.

 

Ili kujiepusha na israfu, kwa mfano, kama una kiu kidogo, basi weka maji kiasi tu cha kumaliza kiu chako.  Usije kujaza gilasi, maji yakakushinda, kisha ukayamwaga.  Hayo unayoyamwaga ni sehemu ya Neema ya Allaah ambayo utakuja kuulizwa Qiyaamah.

 

Tujiepushe na israfu katika vinywaji ili kuidumisha neema hiyo.  Tusishangae kuona nchi mbalimbali zikikabiliwa na ukame wa muda mrefu unaoleta maafa hata kwa mifugo.  Huenda ni baadhi ya matokeo ya israfu zetu.

 

 

 

Share