35-Tukumbushane: Jela Ya Buwlas

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

35:  Jela Ya Buwlas:

 

Wote bila shaka tunaiogopa jela kutokana na madhila na hali mbaya ya kimaisha iliyomo humo.  Kuna jela kwenye baadhi ya nchi zimejaa ukatili na unyama ambao umevuka mipaka yote ya kiutu.  Kuna zingine mtu akiingia huko hatoki tena, na hata akitoka, basi hata jamaa zake wanashindwa kumtambua kutokana na alivyochakarishwa humo.  Hii ni mbali na kukosa uhuru wa mtu aliouzoea, kwani maisha humo ni amri tupu.  Wafungwa wanaweza kuamriwa kulala saa 11 jioni na kuamka saa 10 alfajiri.  Lakini kutokana na hali hiyo, inabidi kuzoea tu.

 

Hii kwa kifupi ndio jela ya dunia.  Sasa huko aakhirah, kuna jela inayojulikana kama “BUWLAS”.  Jela hii ni mahususi kwa wote wenye kiburi hapa duniani. Kiburi maana yake ni kuikataa haki iliyo dhahiri yenye ushahidi kamili.  Ni kama Firauni alivyokataa kumwamini Muwsaa (‘Alayhis Salaam) pamoja na muujiza aliouona ambao uliwafanya wachawi mabingwa waamini na kuporomoka kusujudu.  Kiburi pia ni kuwadharau watu kutokana na hali aliyonayo mtu ya utajiri, au cheo, au mamlaka, au elimu, au utaifa, ukabila na kadhalika.  Wote wenye tabia hizi, basi wanasubiriwa na jela hii ya “Buwlas”.

 

Jela hii ikoje?  Wenye kiburi watafufuliwa vipi Siku ya Qiyaamah kabla ya kuswekwa humo?  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:

 

"يُحْشَرُ الْمُتَكَبِّرُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَمْثَالَ الذَّرِّ فِي صُوَرِ الرِّجَالِ، يَغْشَاهُمُ الذُّلُّ مِنْ كُلِّ مَكَانٍ، فَيُسَاقُونَ إِلَى سِجْنٍ فِي جَهَنَّمَ يُسَمَّى بُولَسَ، تَعْلُوهُمْ نَارُ الأَنْيَارِ يُسْقَوْنَ مِنْ عُصَارَةِ أَهْلِ النَّارِ طِينَةِ الْخَبَالِ ‏"‏.‏ قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ.‏

 

“Wenye kiburi watakusanywa Siku ya Qiyaamah (kwenye uwanja wa mahshar) wakiwa mfano wa chembe ndogo mno iliyo katika umbo la mwanaume, na watafunikwa na udhalili kutoka kila mahali.  Halafu wataswagwa kupelekwa kwenye jela iliyoko ndani ya Jahannam iitwayo “Buwlas”.  Moto wa mioto utawafunika juu yao, na watanyweshwa usaha na taka mwili za watu wa motoni (ambazo ni) “Twiynatul Khabaal”.  [At-Tirmidhiy: (2492)]

 

Watakuwa wanakanywagwa na watu hapo ikiwa ni malipo ya mfano wa kiburi walichokuwa nacho hapa duniani.

 

Tusisahau kwamba neema zote tulizonazo tumetunukiwa na Allaah kama majaribio.  Tusije kujisahau tukaingia kwenye kundi hili tukaishilia kusekwa kwenye jela ya “Buwlas”.

 

 

 

Share