36-Tukumbushane: Walevi Nao Wanasubiriwa Na “Twiynatul Khabaal”

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

36:  Walevi Nao Wanasubiriwa Na “Twiynatul Khabaal”:

 

Pombe inavyoonekana ni suala ambalo limekuwa la kawaida.  Tumewahi kuwasikia hata baadhi ya Waislamu tena wenye umaarufu mkubwa wakikiri hadharani kwamba wanakunywa.  Hawa ima nyoyo zao zishasusuwaa; hawajali tena wala kumwogopa Allaah, au pengine hawajui hatari ya hatima mbaya inayowasubiri kesho aakhirah.

 

Pombe yenyewe kwanza imelaaniwa pamoja na wadau wake wote akiwemo mtengenezaji, mnywaji, mnunuzi, mhudumu na kadhalika.  Na laana watu wanaichukulia kama ni kitu kidogo tu.  Laana maana yake ni kuwekwa mbali na Rahma ya Allaah kama ilivyomtokea Ibliys, na hatima yake ni motoni tu, na anayekunywa au kuhusika nayo kwa namna moja au nyingine, basi hatima yake ni sawa na ya Ibliys.

 

Isitoshe, huko ndani ya moto wa Jahannam, wanywaji pombe watanyweshwa kile alichokiita Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni “Twiynatul Khabaal” pale aliposema:

 

"كُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ، إِنَّ عَلَى اللَّهِ عَهْدًا لِمَنْ يَشْرَبُ الْمُسْكِرَ أَنْ يَسْقِيَهُ مِنْ طِينَةِ الْخَبَالِ. قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا طِينَةُ الْخَبَالِ؟ قَالَ: عَرَقُ أَهْلِ النَّارِ أَوْ عُصَارَةُ أَهْلِ النَّار"

 

“Kila kinacholewesha ni haramu.   Na kwa hakika Allaah Amemwekea ahadi mwenye kunywa chenye kulewesha kwamba Atamnywesha “Twiynatul Khabaal”.   Wakauliza ni nini  “Twiynatul Khabaal?”.   Akasema:   Ni jasho la watu wa motoni, au ni usaha wa watu wa motoni”.   [Hadiyth Swahiyh.   Imekharijiwa na Muslim (2002), An Nasaaiy (8/327) na Ahmad (3/321)].

 

 

 

Share