37-Tukumbushane: Tusipoteze Nafasi Hii Ya Kuombewa Maghfirah
Tukumbushane
37: Tusipoteze Nafasi Hii Ya Kuombewa Maghfirah:
Kati ya Fadhila kubwa kabisa za Allaah kwetu sisi kama Waumini, ni kuwafanya Malaika Wake Watukufu watuombee maghfirah Kwake na Atukinge sisi na adhabu ya Jahiym. Malaika hawa ni wengi kuliko wanadamu kwa idadi kubwa mno ambayo hakuna aijuaye ila Allaah Mtukufu. Na kwa wingi huu, kwa hakika, Waislamu watakuwa wananufaika sana kutokana na du’aa za Malaika hawa wote ambao daima humsabbih Allaah na kumhimidi.
Wanaoongoza kwa duaa hiyo ni Malaika wabebao ‘Arshi ya Allaah ambayo ndio kiumbe kikubwa zaidi kuliko vyote, kizuri kuliko vyote na kilicho karibu zaidi kwa Allaah Ta’aalaa. ‘Arshi hii Tukufu imeenea ardhi yote, mbingu zote, pamoja na Kiti Chake. Malaika hawa kupewa kazi hii ya kubeba ‘Arshi inaonyesha kuwa ndio Malaika wakubwa zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko viumbe wote. Na Allaah kuwachagua kubeba ‘Arshi hii, inaonyesha kuwa wao ndio Malaika bora kabisa kuliko wengineo, nao ndio walio karibu zaidi na Allaah.
Lakini, ni yepi masharti ya sisi kuweza kunufaika na tunukio hili na takrima hii kubwa kabisa ya Allaah ya kuombewa maghfira na rahmah na Malaika hao wabebao ‘Arshi na wengineo walio pembezoni mwake? Jibu la swali hili liko katika Aayah hii ya saba ya Suwrat Ghaafir:
"الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ"
“(Malaika) ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih na kumhimidi Rabbi wao, na wanamwamini, na wanawaombea maghfirah wale walioamini (wakisema): Rabb wetu! Umekienea kila kitu kwa rahmah na ujuzi, basi Waghufurie wale waliotubu, na wakafuata Njia Yako, na Wakinge na adhabu ya moto uwakao vikali mno”. [Ghaafir: 07]
Masharti haya ni:
Kwanza: Kuwa na iymaan ya kikweli mbali na unafiki na shirki.
Pili: Kutubia toba ya kikweli kwa kila kosa kwa masharti yake manne yajulikanayo. Mtu atubie kila anapofanya kosa, kwani mwanadamu ni mkosaji wa mara kwa mara.
Tatu: Kufuata kikamilifu Njia ya Allaah kwa uthabiti na uimara kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.
Tukitekeleza masharti haya, basi tutaingia moja kwa moja ndani ya duara hili. Hakika Mapenzi ya Allah kwa Waumini ni makubwa sana. Na tukijaaliwa kuingia, hivi kuna dhambi tutabaki nalo?