38-Tukumbushane: Baadhi Ya Vitendo Vinavyoingiza Ndani Ya Duara La Kuombewa Maghfirah Na Malaika

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

38:  Baadhi Ya Vitendo Vinavyoingiza Ndani Ya Duara La Kuombewa Maghfirah Na Malaika:

 

Haya ni miongoni mwa mambo mengineyo ambayo yatakuingiza ndani ya wigo wa kuombewa maghfirah na Malaika.

 

1- Kusubiri swala ya jamaa msikitini na kukaa baada ya kumalizika swala. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"إِنَّ الْمَلاَئِكَةَ تُصَلِّي عَلَى أَحَدِكُمْ مَا دَامَ فِي مُصَلاَّهُ الَّذِي صَلَّى فِيهِ مَا لَمْ يُحْدِثِ : اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ، اللَّهُمَّ ارْحَمْهُ"

 

“Hakika Malaika wanamwombea mmoja wenu madhali amebakia sehemu yake aliyoswalia na kuwa hajatengukwa na wudhuu wake. (Wanasema):  Ee Allaah, Mghufurie, ee Allaah Mrehemu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (659) na Muslim (649)]

 

Mwanamke anaweza kuipata fadhila hii kama atakuwa na sehemu yake mahsusi ya kuswalia nyumbani kwake.

 

2-  Kuswali safu ya kwanza.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  anasema:

 

"إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الصَّفِّ الْأَوَّلِ"

 

“Hakika Allaah na Malaika Wake Huwaswalia wanaoswali safu ya kwanza”.  [Hadiyth Swahiyh.  Swahiyh Ibn Maajah]

 

Kuwaswalia hapa kuna maana ya kwamba, kwa upande wa Allaah ni kuwasifu na kuwarehemu, na kwa Malaika ni kuwaombea maghfirah.

 

Baadhi ya Waumini utawaona wamewahi kuingia msikitini na safu ya kwanza haina watu.   Badala ya kuwahi na kukaa safu hiyo ili wapate fadhila hii, hukaa safu za nyuma.  Pengine hawajui fadhila hii, au wanaona safu ya kwanza ni ya watu maalum.  Hili ndilo la watu kulishindania, kwani kheri zake ni kubwa.

 

3-  Kutafuta ‘ilmu.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"مَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَطْلُبُ فِيهِ عِلْمًا سَلَكَ اللَّهُ بِهِ طَرِيقًا مِنْ طُرُقِ الْجَنَّةِ وَإِنَّ الْمَلاَئِكَةَ لَتَضَعُ أَجْنِحَتَهَا رِضًا لِطَالِبِ الْعِلْمِ وَإِنَّ الْعَالِمَ لَيَسْتَغْفِرُ لَهُ مَنْ فِي السَّمَوَاتِ وَمَنْ فِي الأَرْضِ وَالْحِيتَانُ فِي جَوْفِ الْمَاء"

 

“Mwenye kupita njia kwa lengo la kutafuta ‘ilmu, basi Allaah Atampitisha kwayo njia katika njia za Peponi.  Na kwa hakika Malaika hushusha mbawa zao kuonyesha kufurahishwa kwao na mwanafunzi mtafutaji ‘ilmu.  Na kwa hakika (pia), aliyeelimika, huombewa maghfirah na walioko mbinguni na walioko ardhini, na (hata) samaki walioko ndani ya kina cha maji”.  [Sunan Abu Daawuwd].

 

Angalia hapa, si tu kwamba anapewa hishma kubwa na Malaika ya kushushiwa mbawa zao, bali hata viumbe vyote vilivyoko mbinguni kati ya Malaika wengineo wakiwemo wale wabebao ‘Arshi ya Allaah, pamoja na viumbe vinginevyo tusivyovijua huko, mbali na viumbe vyote vilivyoko ardhini hata vile tunavyovidharau kama nzi, panya, chawa na kadhalika, isitoshe na vyote vilivyoko ardhini, -vyote hivyo kwa wingi wote huo wa idadi isiyoweza kukokotoleka- vinamwombea maghfirah mwanafunzi anayetafuta ‘ilmu.  Na ‘ilmu inayolengwa hapa ni ‘ilmu ya dini, kwani hiyo ndiyo itakayomwongoza Muislamu katika ‘aqiydah safi, atajua vyema mambo yote ya ‘ibaadah kuanzia twahara, swala, zakah, funga, hijja na mengineyo yote kuhusu kusoma Qur-aan kama inavyotakikana, Hadiyth za Rasuli na kadhalika.  Haya ndiyo yatakayomfanya kuishi kwa amani hapa duniani na kesho aakhirah.

 

Ama elimu za kidunia, hizi bila shaka mtu atazijua tu kwa mujibu wa utashi wake katika kutafuta riziki.  Na hizi ndizo ambazo watu wamezipa kipaumbele zaidi kuliko za dini.  Si ajabu ukamwona mhandisi mkubwa au mwanasiasa mashuhuri wa Kiislamu, lakini kwa upande wa dini yake, ni mtupu kabisa!  Hii ni hasara kubwa itakayomfanya Muislamu yeyote asiyetafuta ‘ilmu ya dini, kuja kujuta sana Siku ya Qiyaamah.

 

4-  Kufundisha watu mambo ya kheri.

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"إِنَّ اللَّهَ وَمَلاَئِكَتَهُ وَأَهْلَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ حَتَّى النَّمْلَةَ فِي جُحْرِهَا وَحَتَّى الْحُوتَ لَيُصَلُّونَ عَلَى مُعَلِّمِ النَّاسِ الْخَيْرَ"

 

“Hakika Allaah na Malaika Wake, pamoja na wakazi wa mbingu na ardhi, hata mdudu chungu katika shimo lake, na hata samaki, wanamwombea mwenye kuwafundisha watu mambo ya kheri”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2685) na At-Twabaraaniy (8/278)]

 

Mwalimu wa mambo ya kheri anayekusudiwa hapa ni Mwanachuoni, kwani yeye huwafundisha watu Maamrisho ya Allaah na kuwaonyesha Makatazo Yake ili wayaepuke, na mambo mengineyo yatakayowafaa katika dunia yao na aakhirah yao.

 

Ni wangapi kati yao wameshafariki zamani, lakini elimu zao hadi leo zinaendelea kuwanufaisha Waislamu.  Na hii ina maana kuwa bado nao wanaendelea kuombewa na wote waliotajwa katika Hadiyth hii ingawa wako makaburini!

 

Lakini pia, hata yeyote anayesambaza elimu ya dini kwa njia ya mitandao kama tunavyoona vijana wetu hivi leo, basi wanaingia ndani ya duara la wigo huu, kuanzia wanaotarjumi, wanao-edit, wanaosambaza na kadhalika.  Allaah Awalipe wote jazaa njema.

 

5-  Kumswalia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُصَلِّي عَلَىَّ إِلاَّ صَلَّتْ عَلَيْهِ الْمَلاَئِكَةُ مَا صَلَّى عَلَىَّ فَلْيُقِلَّ الْعَبْدُ مِنْ ذَلِكَ أَوْ لِيُكْثِرْ"

 

“Hakuna Muislamu yeyote anayeniswalia isipokuwa Malaika nao humswalia madhali anaendelea kuniswalia.  Basi na mja afanye uchache kwa hilo, au akithirishe”.   [Hadiyth Hasan.  Ibn Maajah]  

 

6-  Kumzuru mgonjwa

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"مَا مِنْ رَجُلٍ يَعُودُ مَرِيضًا مُمْسِيًا إِلاَّ خَرَجَ مَعَهُ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ يَسْتَغْفِرُونَ لَهُ حَتَّى يُصْبِحَ وَكَانَ لَهُ خَرِيفٌ فِي الْجَنَّةِ وَمَنْ أَتَاهُ مُصْبِحًا خَرَجَ مَعَهُ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ يَسْتَغْفِرُونَ لَهُ حَتَّى يُمْسِيَ وَكَانَ لَهُ خَرِيفٌ فِي الْجَنَّةِ"

 

“Hakuna mtu yeyote anayemzuru mgonjwa wakati wa jioni, isipokuwa hutoka pamoja naye Malaika elfu sabini wanaomwombea maghfira mpaka apambaukiwe asubuhi, na atapata pia bustani iliyosheheni matunda Peponi.  Na atakayemwendea asubuhi, hutoka pamoja naye Malaika elfu sabini wanaomwombea maghfira mpaka jioni, na atapata bustani iliyosheheni matunda Peponi”.   [Hadiyth Hasan.  Swahiyh Abu Daawuwd]

 

7-  Wanaokula daku

 

Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"إنَّ اللهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّوْنَ عَلَى المُتَسَحِّرِيْنَ"

 

“Hakika Allaah na Malaika Wake wanawaswalia wenye kula daku”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Ibn Hibaan (3467)]

 

Kuswaliwa na Allaah kuwasifu na kuwarehemu, na Malaika ni kuombewa maghfirah kwa Allaah.

 

Daku ni barakah.   Si lazima kula mlo kamili wa shibe, bali inatosha hata kwa funda la maji ili kupata kusifiwa na Allaah na kuombewa maghfirah na Malaika Wake.

 

 

Share