39-Tukumbushane: Laiti Ningelikuwa Mkia Wa Mbwa

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

39:  Laiti Ningelikuwa Mkia Wa Mbwa:

 

Kuna baadhi ya viumbe vya Allaah ambavyo tunavichukia na hata kuvilaani kutokana na madhara yake kama nzi, mbu, kunguni, na kadhalika.  Viumbe hivi Allaah Ameviumba kwa sababu na hekima maalum ambazo ni vigumu sisi kuzijua.  Na hata kuna wanyama wengine ambao tunawadharau kiasi cha hata kufanywa kama ni tusi kwetu.  Ni kama mtu kumwambia mtu:  “Wewe punda tu”, au “Wewe mbwa tu”, au “Wewe kenge tu”.  Hili ni kosa kubwa la kuwadharau viumbe hawa wa Allaah, na inakuwa ni kama kumdharau Yeye, na hii ni hatari kubwa sana.

 

Pamoja na kuwadharau wanyama hawa, lakini kuna siku mtu atakuja kutamani laiti yeye angelikuwa mbwa au punda au hata nguruwe.  Hawa ni wale watakaojikuta Siku ya Qiyaamah wakisubiriwa na hatima mbaya ya kuishilia motoni.

 

Siku hii, wanyama hawa wote watafufuliwa ili walipiziwe kisasi kati yao.   Kondoo mwenye pembe aliyempiga mwenzake asiye na pembe, atalipiziwa naye kwa kupigwa pembe.  Aliyemparua mwenzake kwa kucha au meno, naye ataparuliwa na kadhalika.  Na hii yote, ni Allaah kuonyesha uadilifu Wake uliofikia ukamilifu wa juu kabisa kwa kila kitu.  Na baada ya visasi kumalizika kwa wanyama wote, hapo Allaah Atawaamuru wawe mchanga, nao watageuka kuwa mchanga.  Kafiri au mtu aliyejaa madhambi, atatamani hapo laiti angeliumbwa mchanga hapa duniani, au hata wanyama hao ili yasimkute magumu yanayomsubiri mbele yake.  Atatamani angelikuwa hata angalau mkia wa mbwa, au sikio la nguruwe hapa duniani, kwa kuwa angelipona Siku hiyo. Lakini wapi!!

 

Allaah Anatuambia:

 

"إِنَّا أَنذَرْنَاكُمْ عَذَابًا قَرِيبًا يَوْمَ يَنظُرُ الْمَرْءُ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ وَيَقُولُ الْكَافِرُ يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا"

 

 

Hakika Sisi Tumekuonyeni adhabu ya karibu.  Siku mtu atakapotazama yale iliyokadimisha mikono yake, na kafiri atasema:  Laiti ningelikuwa mchanga”. [An-Nabaa].

 

Tuheshimu sana viumbe vyote vya Allaah.  Kuviheshimu ni sehemu ya kumheshimu Allaah Aliyeviumba na kuvisakharisha kwa ajili ya maslaha yetu.

 

 

 

Share