40-Tukumbushane: Je, Mamba anafaa Kwa Kitoweo?

 

Tukumbushane

 

Alhidaaya.com

 

 

 

40:  Je, Mamba anafaa Kwa Kitoweo?

 

Kuna makhitilafiano baina ya ‘Ulamaa kuhusiana na uhalali na uharamu wa kula nyama na mamba.

 

Kundi la wenye kuhalalisha ambao ni pamoja na Jopo la Tume Ya Fatwaa Ya ‘Ulamaa wa Saudia wanasema naam, mamba anafaa kuliwa kama anavyoliwa samaki.   Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa :

 

"أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ"

 

“Mmehalalishiwa mawindo ya bahari, na chakula chake ni manufaa kwenu na kwa wasafiri”.   [Al-Maaidah: 96]

 

Na kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 "هُوَ الطَّهُورُ مَاؤُهُ الْحَلاَلُ مَيْتَتُهُ"

 

“(Bahari) maji yake ni twahara, na maiti yake ni halali”.   [Sunan An-Nasaai (4550].

 

Wanyama wote wanaoishi majini ni halali kuliwa akiwemo mamba.  Si lazima iwe ni bahari tu, bali kwenye mito, maziwa na kadhalika.

 

Ama kundi la pili la walioharamisha kula mamba, wao wanasema kwamba  mamba ana meno makali ya kukamatia kiwindwa chake, na Rasuli amekataza kula nyama ya wanyama au ndege wakali wanaotumia meno au kucha kuulia viwindwa vyao kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:

 

"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ ُ َكُلِّ  ذِيْ نَابٍ مِنَ السِّبَاعِ، وَعَنْ كُلِّ ذِيْ مِخْلَبٍ مِنَ الطَّيْرِ"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila mwenye meno katika wanyama wakali, na kila mwenye kucha katika ndege”.  [Hadiyth Swahiyh.   Imekharijiwa na Muslim (1934), Abu Daawuwd (3785) na An Nasaaiy (7/206)].

 

Kadhalika, wanasema kwamba mamba yuko nusu nusu; nchi kavu na majini, hivyo hawezi kuchukuliwa kuwa ni wa majini tu ili apewe uhalali wa kuliwa.

 

Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah) amewajibu kwamba ndani ya bahari kuna samaki wakubwa wenye meno ya kutisha zaidi kama nyangumi, papa na kadhalika.   Lakini hao wanaopinga wamehalalisha kuliwa samaki hao.   Kwa nini waharamishe mamba?   Halafu, mamba si kama wanyama wakali wa nchi kavu, na kwa hivyo basi, si kila cha nchi kavu kinachoharamishwa kiharamishwe mfano wake wa kilichoko majini.   Isitoshe, muda wake mwingi huwa majini kuliko nchi kavu, na wingi hutangulizwa kuliko uchache.

 

Hayo ndio makhitilafiano kidogo kuhusu uhalali na uharamu.  Angalia mwenyewe na upime, kisha chukua uamuzi.

 

 

Share