42-Tukumbushane: Vipi Na Chura?
Tukumbushane
42: Vipi Na Chura?
Chura ni haramu kumla, kwa sababu Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuua vyura. Qaaidah inasema:
“Mnyama Ambaye Allaah Au Rasuli Wamekataza Kumuua Si Halali Kuliwa”.
Ni kama sisimizi, nyuki, hud-hud, tiva (shrikes) na chura. Ni kutokana na Hadiyth hii ya Ibn ‘Abbaas ambaye amesema:
"نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ قَتْلِ أَرْبَعِ مِنْ اَلدَّوَابِّ : اَلنَّمْلَةُ، وَالنَّحْلَةُ، وَالْهُدْهُدُ، وَالصُّرَدُ".
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuua viumbe wanne: Sisimizi, nyuki, hud-hud na tiva (shirkes)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (5/189), Ahmad (6/83) na wengineo].
Hawa wote watajwa hapa, hairuhusiwi kuwaua, hairuhusiwi kuwala.
Ama katazo la kuua chura na kuwa haramu kuliwa, ni kwa Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin ‘Uthmaan ambaye amesema:
"ذَكَرَ طَبِيبٌ عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ دَوَاءً، وذَكَرَ الضِّفْدَعً يَجْعَلُ فِيْهِ، فَنَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ قَتْلِ الضِّفْدَع"
“Tabibu (daktari) alitaja mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dawa, na akaeleza kwamba dawa hiyo anaitengeneza kutokana na chura. Na hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakataza kuua chura”. [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad (15197), Ad-Daaramiy (1998) na Ibn Maajah (3223)].
Kwa msingi huu, chura haliwi wala hawindwi.